Friday, October 4, 2019



Yanga imelazimishwa sare ya mabao 3-3 dhidi ya Polisi Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam leo.

Yanga ndiyo waliokuwa wa kwanza kuandika bao la mapema mnamo dakika ya 6 kupitia kwa Mrisho Ngassa baada ya kupokea krosi safi kutoka kwa Juma Abdul aliyeipiga kulia mwa uwanja.

Polisi walijibu mapigo mnamo dakika ya 34 kipindi cha kwanza kupitia kwa Ditram Nchimbi aliyeingia kambani mara tatu leo.

Mpaka dakika 45 za kwanza zinamalizika, Yanga na Polisi wakuwa sawa kwa matokeo ya 1-1.

Mnamo kipindi cha pili Polisi walikuja juu na kuandika bao la pili kupitia kwa yuleyule Nchimbi aliyefunga baada ya kupokea pasi safi iliyopenyezwa katikati mwa uwanja kumfunga kiufundi kipa Metacha Mnata ikiwa ni dakika ya 55.

Na katika dakika ya 58 tena, Nchimbi aliingia tena kambani akifunga mpira wa kichwa na kufanya matokeo yawe 3-1.

Yanga waliamka tena kwa kasi ya ajabu ambapo David Molinga 'Falcao' alifunga katika dakika ya 65 baada ya kipa wa Polisi, Kulwa Manzi kushindwa kuumiliki mpira vizuri baada ya kumponyoka na kuelekea nyavuni.

Mnamo dakika ya 69 tena, Molinga aliingia tena kambani kupitia mpira wa faulo ambao ulimzidi nguvu kipa wa Polisi, na mpaka kipyenga kinamalizika, matokeo ni 3-3.

0 comments:

Post a Comment