
Mturuki Ramil Guliyev alitamatisha
ndoto za bingwa wa mbio za mita 400 duniani Wayde van Niekerk na raia wa
Botswana Isaac Makwala kwa kushinda taji la dunia la mbio za 200m
Alhamisi usiku.
Raia wa Afrika Kusini Van Niekerk alikuwa akitaka
kushinda 200m na 400m wakati mmoja kwa mara ya kwanza tangu Michael
Johnson alipofanya hivyo miaka 22 iliyopita.Makwala naye alikuwa amekimbia peke yake nusu fainali kufuzu baada yake kuzuiwa kushiriki kwa njia ya utata kwa sababu za kiafya.
Lakini Guliyev, 27, aliyekuwa raia wa Azerbaijan lakini akabadilisha uraia wake 2011, alistahimili upinzani mkali kutoka kwa Van Niekerk (aliyetumia sekunde 20.11) na Jereem Richards wa Trinidad na Tobago (20.11) na kuishindia Uturuki dhahabu yake ya kwanza katika mashindano ya sasa ya Ubingwa wa Dunia yanayoendelea jijini London kwa muda wa 20.09.
"Haijanishangaza sana," alisema baada ya kushinda. "Lakini haonekani kama ni kweli.

"Nimejikakamua sana muda wote katika mashindano haya. Nilijizatiti zaidi wakati ufaao. Nina furaha sana kuwa bingwa wa dunia. Huu ndio wakati bora zaidi katika maisha yangu katika riadha."
Makwala alikuwa amegeuka shujaa wa London 2017 baada ya kuzuiwa kushiriki mbio za kufuzu fainali mbio za 400m na 200m baada ya maafisa wa matibabu wa IAAF kumtenga kwa saa 48 wakihofia alikuwa ameambukizwa virusi, lakini hakuwa na virusi hivyo vya norovirus.

0 comments:
Post a Comment