Saturday, September 1, 2018






Mlinzi aliyefanikiwa kuwakaba washambuliaji Heritier Makambo wa Yanga na Meddie Kagere wa Simba, Kassian Ponela wa Mtibwa Sugar, amesema baada ya kuwavaa nyota hao anaona Makambo ni bora zaidi.


Washambuliaji hao kwa sasa ni gumzo kutokana na kuanza ligi kwa kasi kubwa, Kagere ndiye kinara wa mabao Simba akiwa nayo matatu aliyofunga kwenye mechi mbili na Makambo amefunga bao moja tu. 

Ponela amesema kuwa Makambo ambaye alifanikiwa kucheza naye kwenye mechi ya ligi kuu msimu huu, ana nguvu na anajua kupambana na mabeki ukilinganisha na Kagere pamoja na Emmanuel Okwi wanaocheza Simba.

Beki huyo wa kati aliongeza kuwa alipata shida sana kumkaba Makambo alipokutana naye na alijitahidi kumzuia asifunge lakini alishindwa kutokana na uwezo mkubwa alionao mchezaji huyo.


“Kwangu mimi namuona Makambo kuwa ni bora  zaidi, nasema hivyo kwa sababu ana kila kitu anachotakiwa kuwa nacho mshambuliaji, ana nguvu, kasi, uwezo wa kumiliki mpira, anajua kupiga chenga lakini pia siyo muoga wa kupambana na mabeki wakorofi.


“Okwi yeye ni mzuri, ana kasi na anajua kumiliki mpira lakini hana nguvu pia ni muoga wakati Kagere yeye siyo muoga, ana nguvu, kasi na uwezo wa kupambana lakini siyo mzuri sana katika kumiliki mpira na kupiga chenga, kwa hiyo Makambo yupo vizuri,” alisema Ponela.

0 comments:

Post a Comment