STRAIKA
wa Yanga, raia wa DR Congo, David Molinga, ametimkia nchini na kwenda
zake Ufaransa kwa madai ya kwenda kutatua matatizo ya familia yake
ambayo inaishi nchini humo.
Tangu Molinga atue Yanga
msimu huu, ameshafunga mabao manne kwenye Ligi Kuu Bara, pamoja na
kudaiwa kutochezeshwa mchezo wao dhidi ya Simba uliopigwa Jumamosi
iliyopita kufuatia kile kilichodaiwa kusimamishwa na uongozi huo kwa
utovu wa nidhamu aliouonyesha baada ya kufanyiwa mabadiliko kwenye
mchezo wao dhidi ya Biashara United.
Chanzo
chetu kimeliambia Championi Jumatano kuwa, kutokana na adhabu hiyo
Molinga aliendelea kuonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu jambo ambalo
limesababisha atupwe nje ya kikosi hicho kiasi cha kuamua kutimkia
nchini Ufarasa kuonana na familia yake.
“Molinga
hayupo kikosini kwetu tangu tuje hapa Unguja, ila kwa dalili
ninazoziona sidhani kama kweli atarejea tena ndani ya kikosi maana
amekuwa na tofauti na viongozi tangu siku ile alipofanyiwa mabadiliko
katika mchezo wetu na Biashara, ambapo alitoka na kwenda kuvaa nguo zake
za nyumbani kisha akataka kulazimisha kukaa benchi wakati kanuni
haziruhusu kufanya hivyo.
“Nimesikia
ameomba ruhusa ili akatatue matatizo ya kifamilia nyumbani kwake
Ufaransa maana huko ndipo anakoishi na familia yake na kwamba hakai
Congo kama wengi wanavyojua, ninavyoona safari yake hii inaweza kuwa
ndiyo ya moja kwa moja na kwamba inawezekana asirudi tena nchini,”
kilisema chanzo hicho.
Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alipoulizwa kuhusiana na hilo hakuwa tayari kusema chochote.

0 comments:
Post a Comment