TAARIFA KUHUSU SERENGETI BOYS
Kuna taarifa zimekuwa zikienea na
kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii, zikidai kuwa Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) limewatelekeza wachezaji wa timu ya mpira wa
miguu ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17.
Wadai kwamba eti hawakulipwa posho na kushutumu viongozi wa juu wa shirikisho kuhusu jambo hilo. Hizi taarifa si za kweli.
Aidha, Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), linapenda kuwajulisha wazazi na umma kwa ujumla
kwamba vijana wetu walilipwa posho zao zote wakiwa kambini Morocco na
Cameroon na zile za mashindano ya AFCON nchini Gabon.
Vilevile, Shirikisho linafanya
taratibu za kupeleka maombi kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu
(Football Development Fund FDF) ili kuweza kuwalipa vijana na benchi la
ufundi sehemu ya posho zilizokuwa bado hazijakamilishwa wakati wa
michuano ya kufuzu kwa AFCON 2017.
Tumeshtushwa na taarifa hizo
ambazo tafsiri yake ni kuharibu uhusiano mwema kati ya shirikisho,
wazazi na wachezaji ambao wanatarajiwa kuitumikia timu ya Taifa ya
Vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 maarufu kama Ngorongoro Heroes.
Shirikisho linaendelea kuwatambua
vijana wa Serengeti Boys kwani bado ni sehemu ya kikosi cha Ngorongoro
Heroes na hivyo ukifika wakati wataitwa kambini kwa ajili ya michezo ya
kimataifa ya U-20.
TFF inazidi kuushukuru umma ambao
umeendelea kuchangia Mfuko wa FDF ambao kimsingi kazi yake ni kutafuta
rasilimali kwa ajili ya maendeleo ya mpira.
Tunaomba michango iendelee kwani
bado tuna changamoto za mashindano mbalimbali kwa timu za wanawake na
vijana ikiwemo fainali za wanawake Afrika zitakazofanyika Ghana hapo
mwakani kwa timu ya Twiga Stars na AFCON 2019 kwa Serengeti Boys ambayo
itakuwa mwenyeji.
Mfuko wa Maendeleo ya Mpira – FDF
ulianzishwa kwa lengo la kutafuta rasilimali za maendeleo ya mpira wa
miguu hasa kwa wanawake na vijana pamoja na miundombinu ya mchezo huo.
Mfuko huo uko chini ya Mwenyekiti
Bw. Tido Mhando anayeongoza Bodi na Mtendaji Mkuu (CEO) ni Bw. Dereck
Murusuri anayesimamia sekretarieti.
0 comments:
Post a Comment