Timu ya riadha ya vijana chini ya
miaka 17 imeleta heshima kubwa kwa nchi yetu baada ya kurejea na medali
ya shaba aliyoshinda kijana Francis Damasi katika mbio za mita 3000
kwenye mashindano ya Jumiya ya Madola yaliyomalizika hivi karibuni
huko nchini India.
Timu hiyo iliyorejea nchini leo
imepokelewa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo
Prof Elisante Ole Gabriel katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa
Mwalimu Julius Nyerere ambapo ameeleza kufurahishwa na matokeo hayo
mazuri waliyopata wanariadha hao ambao wameitangaza vyema Tanzania.
“Vijana mmefanya vizuri sana
katika mashindano haya Serikali tunawapongeza sana kwa kuitangaza nchi
yetu lakini pia kwa kuonyesha uzalendo wa hali ya juu katika mashindano
haya nawaahidi kuendelea kushirikiana na uongozi na wadau wa riadha
nchini ili tufike mbali zaidi” Alisema Prof. Elisante Ole Gabriel.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa
chama cha riadha nchini Bw. Filbert Bayi amesema kuwa mchezo wa riadha
kwa sasa ni mchezo ambao umeitangaza Tanzania kwa kiasi kikubwa kutokana
na kushiriki mashindano mengi ya Kimataifa hivyo ni vyema wadau
wakajitokeza kwa wingi kuwekeza katika mchezo huo ambao umeendelea
kuletea heshima Taifa.
“Riadha imeitangaza Tanzania na
itaendelea kuitangaza hivyo wadau wanapaswa kuona fursa hii na kuwekeza
katika mchezo huu ili ufike mbali,kila mtu katika eneo lake aone fursa
hii na aitumie kwa manufaa ya kizazi hiki na kitakachokuja” Alisema Bw.
Bayi.
Naye Kijana Francis Damian
aliyepata medali hiyo baada kushinda mbio za mita 3000 ameeleza
kufurahishwa na ushindi huo kwani alijiandaa na alizingatia maelekezo ya
walimu wake yaliyompelekea kupata ushindi huo na ameshauri vijana kama
yeye kuthubutu na kuamini kuwa wanaweza kwani mchezo huo ni mzuri na una
mafanikio makubwa.
Medali ya shaba katika mahindano
ya riadha iliyoletwa na kijana Francis imerejea tena baada ya miaka 19
tangu Tanzania ilivoshinda medali hiyo mwaka 2008.
0 comments:
Post a Comment