Saturday, October 14, 2017


KAMA wanahitaji kupata ushindi katika mchezo wa Jumamosi hii ni lazima kikosi cha Yanga kibadilike kimbinu na kiufundi wakati watakapoivaa Kagera Sugar FC katika uwanja wa Kaitaba, Bukoba. Kama wanataka ubingwa wanne mfululizo ni lazima wachezaji ‘wanyanyuke’ kuanzia mchezo wa raundi ya sita wikendi hii na kucheza kama mabingwa wa kweli watetezi.
Michezo mitano iliyopita kwa mabingwa hao watetezi  ‘imekwenda sawa’ licha ya ukweli tayari wameshaangusha pionti sita huku nne wakifanya hivyo katika uwanja wa nyumbani (Uhuru.) Kufunga magoli manne na kuruhusu mawili katika lango lao ndani ya michezo mitano bado hakuwezi kuondoa sifa ya ‘timu kali’ kiufungaji katika VPL kipindi cha miezi zaidi ya 24.
Bila Ngoma, Kamusoko, ndani ya Kaitaba
Timu kubwa hupata mafanikio kutokana na ‘mihimili isiyotikisika’ lakini sasa Yanga wanakwenda kuivaa Kagera ikiwa bila ya mihimili ya kikosi kilichotamba kwa misimu mitatu iliyopita huku safari yao ya mwisho Kaitaba Stadium mabingwa hao mara 27 wa kihistoria wakishinda 6-2 (ushindi mkubwa zaidi kwa Yanga ndani ya mwaka sasa.)
Kocha wa sasa wa Yanga, Mzambia, George Lwandamina bado  anatafuta namna ya kujiweka sawa tangu alipochukua nafasi ya Hans van der Pluijm mwishoni mwa mwaka uliopita. Anasuka kikosi kipya baada kikosi kilichosukwa na Hans misimu mitatu iliyopita kusambaratika.
Yanga ambayo ilienda kuichapa 6-2 Kagera pale Kaitaba mwaka mmoja uliopita ilikuwa na kundi la wachezaji ‘washindi’, Deo Dida, Ally Mustapha, Mnyarwanda, Mbuyu Twite, Mtogo, Vicent Bossou, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke na aliyekuwa mfungaji bora wa ligi, Saimon Msuva. Hawa wote hawapo hivi sasa na katika soka la ndani naamini wachezaji hawa walikuwa na mchango mkubwa kimbinu na kiufundi katika vikosi vilivyotwaa VPL tatu mfululizo.
Siku nyingi nilikuwa na ‘shahuku’ ya kutaka kuiona Yanga ikicheza ikiwa na wachezaji wengi wazawa katika kikosi chake cha kwanza  na anachojaribu kufanya Lwandamina ni kutengeneza ‘timu bora ya muda mrefu itayotegemea bajeti ndogo ya klabu’
Baada ya sare ya 1-1 nyumbani vs Lipuli FC, ushindi ‘finyu’ wa 1-0 ugenini vs Njombe Mji FC, sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Majimaji FC, ushindi finyu wa kwanza ( 1-0) vs Ndanda FC, kocha Lwandamina aliamua kuanza na wachezaji watatu tu wa kigeni wakati timu yake ilipocheza na Mtibwa Sugar FC katika mchezo wa raundi ya tano huku mchezaji mmoja tu kutoka ng’ambo akiwa katika benchi.
Golikipa,Mcameroon, Youthe Rostand, na washambuliaji, Mzimbabwe, Donald Ngoma na Mzambia, Obrey Chirwa pekee ndiyo walioanza wakati Mzimbabwe, Thaban Kamusoko akiwa katika benchi huku Mrundi, Amis Tambwe akiwa nje kutokana na majeraha yaliyokuwa yakimsumbua.
Imekuwa ngumu kwa Lwandamina kupata huduma ya wachezaji hawa wa kigeni kwa wakati mmoja tangu alipoingia katika timu hiyo mwezi Disemba, 2016. Akiwepo, Ngoma, basi Tambwe atakuwa na tatatizo, akiwepo Chirwa na tatizo Ngoma anaweza kuwa fiti.
Na wakati akiamini kupona kwa Tambwe kungempa nafuu ya uwepo wa washambuliaji wote hao wa kigeni, ila Ngoma ameumia wakati wa mchezo uliopita vs Mtibwa na atakuwa kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar wakati Tambwe aliyekosekana tangu mwanzo wa msimu akitarajia kuungana na kikosi.
Lwandamina anakwenda kuivaa Kagera Sugar ambayo haijapata ushindi wowote ule msimu huu, huku wakiwa mkiani na alama mbili baada ya sare mbili na vichapo vitatu katika michezo mitano iliyopita. Ndiyo, Kagera wamefunga goli moja tu na kuruhusu manne jambo ambalo linaweza kuwapa nguvu Yanga kuwa wanakwenda kucheza dhidi ya timu ‘isiyo na makali’ katika ufungaji, na inayopitika katika ngome, ila hii ni mechi ngumu ambayo wachezaji wazawa wanapaswa kuthibisha ubora wao ndani ya Yanga.
Juma Abdul, Gadiel Michael, Vicent Andrew, Kelvin Yondan, Said Juma Makapu, Pius Buswita, Rafael Daud, na Ibrahim Ajib-wote hawa walianza katika mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa na walionyesha ‘mwanga’ mzuri kuwa wanaweza kuibakisha Yanga katika ‘tawi lake’ licha ya changamoto ambazo klabu inapitia kiuchumi.
Bila, shaka kukosekana kwa Kamusoko na Ngoma katika mchezo wa Jumamosi hii imewaongezea hofu mashabiki na wachama wa Yanga, lakini kijana kama Buswita anaweza kufanya kazi ambayo itawashangaza wengi kama ataongeza kasi na umakini wake wakati anaposhambulia kwa pasi zake kwa kwenda mbele.
Buswita alifanya kazi nzuri katika mchezo dhidi ya Mtibwa. Kocha Lwandamina anaweza kunufaika na pasi za kijana huyo kama atasimamisha washambuliaji wawili. Unajua Tambwe, Chirwa na Ngoma wamekuwa katika vipindi vya majeraha mno katika miezi ya karibuni na kitendo cha kutowapanga karibu karibu ni sawa na kuwalazimisha kuumia tena kwa maana watajaribu kufanya kazi ambazo hawataziweza zaidi ya kuwaumiza.
Sasa ni Yanga ya ‘Kitanzania’
Kutumia wachezaji 11 wa Kitanzania katika mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa kuwafumbue macho wachezaji wenyewe na wanapaswa kuamini sasa Yanga inajengwa katika mabega yao na wanaweza kumlinda kocha wao kwa kuifunga tu Kagera kisha Stand United katika wiki ya 7 pale Kambarage Stadium, Shinyanga vinginevyo watakuwa wamejiangusha na kuiangusha klabu.
Hata ukitazama katika mabadiliko mengi ya Lwandamina msimu huu utagundua kuwa Geofrey Mwashuiya, Juma Mahadhi, Emmanuel Martin wamekuwa wakitumika hii inakupa picha halisi ya Yanga jinsi ilivyo hivi sasa. Na hivyo hivyo wanapaswa kupambana kuhakikisha wanapata matokeo katika michezo migumu kama huu vs Kagera Sugar.
Yanga wanatakiwa kushinda tu vinginevyo wataanza kujiondoa wenyewe katika mbio za taji ligi ingali bado mbinchi, kuifunga Kagera Sugar kutawafumbua mamacho wale wanaodai wamekwisha, na wanaweza kwenda kileleni mwa msimamo kwa mara ya kwanza msimu huu kama Azam FC na Singida United zitashindwa kupata ushindi watakapocheza ugenini dhidi ya Ruvu Shooting (Singida) Mwadui FC (Azam FC)

0 comments:

Post a Comment