Bingwa wa Olimpiki Usain Bolt hatimaye atapata fursa ya kuchezea soka katika uwanja wa Manchester United wa Old Trafford.
Mshindi
huyo wa dhahabu mara nane katika Olimpiki atakuwa nahodha wa timu ya
pamoja na watu mashuhuri na wanasoka ambayo itashiriki mechi ya Soccer
Aid ambayo itaandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto
(Unicef) mnamo 10 Juni."Ni ndoto yangu kufanikiwa kama mchezaji wa soka ya kulipwa. Kucheza dhidi ya baadhi ya wachezaji nyota, hilo litakuwa jambo la kufurahisha sana," raia huyo wa Jamaica amesema.
Manchester United wameandika kwenye Facebook: "Inafanyika hatimaye ... Usain Bolt ataonyesha ustadi wake katika kusakata kambumbu katika Old Trafford majira yajayo ya joto #SoccerAid!
Robbie Williams atakuwa nahodha wa timu pinzani kutoka England wakati wa mechi hiyo.

Wikendi, aliandika ujumbe wa utani kwenye Twitter - ambao ulizua uvumi sana - akidokeza kwamba alikuwa amejiunga na klabu fulani.
Bolt, 31, ni shabiki wa Manchester United, na wakati mmoja alipiga simu kwenye runinga ya klabu hiyo, MUTV, bila kutarajiwa.
"Nimekuwa nikisemamuda mrefu kwamba ninataka sana kufanikiwa katika mchezo wa timu kwa sababu uwanjani ni bidii ya mtu binafsi," alisema wakati huo.
"Huwa najiimarisha upesi na kufahamu ninafaa kufanya nini punde ninapopata kazi. Ninapopata maagizo, huyafuatilia vyema sana," alisema.

Mechi hiyo, ambayo huchezwa kila miaka miwili kufikia sasa imechangia kuchangisha jumla ya £24 milioni tangu kuzinduliwa kwake 2006.
Mechi hiyo awali imewashirikisha wachezaji wa zamani kama vile Maradona, Alan Shearer na Ronaldinho wakicheza dhidi ya watu mashuhuri kama vile Mark Wright, Jack Whitehall na Olly Murs.
Will Ferrell, Gordon Ramsay, Mike Myers na Craig David pia wamewahi kucheza.
"Kutwaa tena taji hili kwa niaba ya England litakuwa jambo zuri sana Usain akiongoza Soccer Aid World XI (Timu ya Dunia)," alisema Robbie Williams, ambaye ni mwanzilishi mwenza wa Soccer Aid.
"Nasubiri sana kuongoza timu ya England."
Tiketi za mechi hizo zinauzwa £10 na £50.
0 comments:
Post a Comment