KUNA matawi mengi
maarufu ya Klabu ya Simba, lakini lipo taji moja lina umaarufu mkubwa na
maana kubwa sana kwa mpira wa kisasa. Tawi hilo linaitwa Mpira Pesa.
Hili ni tawi ambalo
hata mashabiki wa Yanga wanatakiwa kulipenda. Ndio, wanatakiwa kulipenda
Tawi la Mpira Pesa. Ni tawi lenye maana kubwa sana kwenye mpira wa
kisasa.
Pamoja na vitu
vingine muhimu sana, lakini mpira unahitaji pesa kwanza. Yanga imepitia
kwenye mikono mingi sana ya watu wenye pesa lakini waliondoka na kuiacha
Yanga masikini.
Yanga haijawahi kuwa tajiri lakini imewahi kuongozwa au kusaidiwa na watu wengi sana wenye pesa.
Wakati Yanga
wanafanya uchaguzi wao huu waliompa Dkt Mshindo Msolla nafasi ya
uenyekiti, nilidhani amekuja kwa jambo moja tu. Nilidhani amekuja kama
msomi kuwapa zawadi wana Yanga.
Yanga kwa zaidi ya
miaka 80 imemkosa mtu wa kuwapa zawadi. Imemkosa mtu wa kuijengea
misingi klabu hii kujitegemea kiuchumi! Hili tu ndiyo jambo kubwa ambalo
Yanga imelikosa kwa miaka yote zaidi 80.
Yanga haijawahi
kushindwa kushinda mataji ya ndani. Yanga haijawahi kukosa mashabiki
kila inakokwenda. Lakini Yanga haijawahi kujitegemea kiuchumi. Ni timu
kubwa inayoishi kwa zaidi ya miaka 80 kwa kutegemea mifuko ya watu
mbalimbali.
Mpira Pesa ni Tawi
la Simba ambalo linaweza kuibadilisha Yanga. Hili tawi lina jina
linalosadifu kitu wanachohitaji Yanga. Kumekuwa na swali gumu sana la
mtu au kampuni inayoweza kuja kuwekeza Yanga baada ya Yusuph Manji
kuiacha Yanga.
Watu wanajiuliza,
hata kama Yanga itakwenda kwenye mfumo wa mabadiliko ya uendeshaji wa
klabu ni tajiri gani yuko tayari kuwekeza Yanga? Hili ni swali ambalo
watu kama GSM waanze kutoa majibu.
Mpira Pesa ndiyo unapaswa kuwa wimbo kwa wana Yanga kwa sasa. Kwa mfumo huu walionao kwa sasa haujawahi kuiacha Yanga tajiri.
Hawa GSM wanakuja
kama alivyokuja Abbas Gulamali, wanakuja kama alivyokuja Manji! Njia ni
zile zile lakini mwenyekiti asipochangamka na kuwatengenezea mfumo wa
uwekezaji wa kisasa na wao wataondoka.
Hata leo hii GSM
wakijitoa Yanga, timu inarudi kulekule! Kazi ya Mwenyekiti wa Yanga kwa
sasa ilipaswa kuwa rahisi tu. Anapaswa kuitisha kikao na kamati yake ya
utendaji na kisha mkutano mkuu wenye lengo la kuwaomba wanachama
wakubali klabu iende kwenye mabadiliko.
Wanachama lazima
wapewe elimu ya kutosha juu ya mabadiliko hayo na waridhie. Bila shaka
yoyote sioni kama wanachama watakataa jambo hili. Angalau kila mwana
Yanga anaona mabadiliko waliyonayo Simba kwa sasa.
Yanga wakiwa makini,
wanaweza hata kufanikiwa zaidi na kwa haraka kuliko hata Simba. Mpira
wa maneno umekwisha, hauwezi kuongoza timu bila pesa.
Kampuni ya GSM ndiyo
inayofanya karibu kila kitu kwa Yanga hii. Kuanzia usajili wa wachezaji
na makocha mpaka mishahara. Ni njia zilezile za kina Abbas Gulamali. Ni
njia zilezile za kina Yusuph Manji. Ni watu wa muhimu sana
kuwashikilia.
Mwenyekiti wa Yanga
asisubiri mpaka na wao wamechoka kumwaga pesa ndiyo akaibuka na hoja ya
mabadiliko. Muda unaokubalika ni sasa. Hakuna mtu aliyefanikiwa
kuiongoza timu ya mpira zama hizi bila kuwa na pesa.
Yanga watakuwa
wanajidanganya kama watakataa mabadiliko. Ni uongo wa levo ya PHD
kuamini kwamba wawekezaji wa wananchi ni wananchi wenyewe.
Hii ni moja ya kauli
mbiu ya uongo kabisa. Yanga imekuwepo miaka zaidi ya 80 kwa wananchi na
hakuna chochote cha kiuchumi kilichowahi kuibeba timu.
Kampuni ya GSM sio wajinga, wanajambo lao. Hakuna mtu kwenye zama hizi ambaye yuko tayari kumwaga pesa tu.
Kila mtu anaijua
pesa. Kila mtu anaipenda pesa. GSM ni wafanyabiashara, kama wana Yanga
wanadhani jamaa wanafaa, wapeni makubaliano ya kibiashara ya uendeshaji
wa klabu yenu.
GSM watakapoona
kwamba hakuna chochote, nao watatoweka. Mwenyekiti wa Yanga huu ndiyo
muda wake wa kumwaga karata dume kwa wanachama. Ndiyo muda wa kuitisha
mkutano mkuu wa wanachama kabla GSM nao hawajakimbia.
Habari za kuendelea
kudanganyana kwamba muwekezaji wa wananchi ni wananchi wenyewe ni uongo
wa daraja la juu sana ambao haujawahi kuisaidia Yanga.
Zama zimebadilika na
Yanga wanatakiwa kubadilika. Narudia, hawa GSM sio wajinga ndiyo maana
ni matajiri. Wanajua kufanya biashara, kama Yanga haiwalipi wanaweza
kuondoka.
Ndiyo tabia za
wafanyabiashara. Hawa ni watu wa kuwashika mkono. Sio lazima hata wapewe
timu peke yao, mnaweza kupata wawekezaji zaidi ya mmoja na wao
wakiwemo.
Kazi ya mwenyekiti
wa klabu kama hana pesa ni lawama tupu. GSM kwa sasa nadhani wanafanya
mambo makubwa kuliko hata kamati ya utendaji ya klabu.
Kwa mpira wa kisasa, unaweza kuwa shabiki wa Yanga, lakini ukalipenda Tawi la Simba la Mpira Pesa!
0 comments:
Post a Comment