Meneja wa bondia wa Cosmass Cheka, Juma Ndambile (kulia) akizungumzia matatizo yaliyompata bondia wake.
Cosmass Cheka akizungumzia hatua
aliyochukuwa ya kukata rufaa BMT kupinga kufungiwa na matokeo ya pambano
lake dhidi ya bondia Haidary Mchanjo.
……………………………..
Na Mwandishi Wetu
Bondia maarufu wa ngumi za kulipwa
nchini, Cosmas Cheka amekata rufaa Baraza la Michezo la Taifa (BMT)
kupinga matokeo na adhabu ya kufungiwa miezi sita na faini ya Sh200,000
iliyotangazwa na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC).
Cheka alisema hayo jana kwenye
mkutano na waandishi wa habari na kusema kuwa TPBC ilikuwa na njama
dhidi yake ili kumtengenezea nafasi bondia Haidary Mchanjo katika ngumi
za kulipwa nchini.
Alifafanua kuwa adhabu dhidi yake
haikufuata sheria kwani kwanza hakupewa nafasi ya kusikilizwa kwa mujibu
wa sheria, huku akimpa nafasi mwamuzi wa pambano hilo, Modest Rashid
ambaye alitaka kupigana naye kuitwa na kujieleza katika kikao cha TPBC.
“Hata kwenye mahakama, lazima
mtuhumiwa apewe nafasi ya kusikilizwa au kujitetea, mimi nilikuwa
ulingoni na mwamuzi na mpinzani wangu Mchanjo, mwamuzi amenitolea maneno
machafu sana, haikutosha akaamua kunikata pointi, niliandika barua ya
kulalamika TPBC, hawajaniita na kuibuka na adhabu kwangu,” alisema
Cheka.
Alisema kuwa pamoja na maamuzi
hayo kutonifikia kimaandishi, nimeamua kuchukua hatua za haraka kwani
tayari vyombo vya habari mbalimbali na mitandaa ya kijamii yamekwisha
tangaza maamuzi hayo yaliyofanywa bila kufuata sheria kwani hawakunipa
nafasi ya kusikilizwa kwa mujibu wa sheria.
Meneja wa bondia huyo, Juma
Ndambile, alisema kuwa walichokifanya TPBC ni kumvunja nguvu bondia wake
ili ashindwe kuendelea na mchezo wake.
Ndambile alisema kuwa TPBC
ilionyesha nia ya kuhujumu matokeo hayo mapema kwa kuweka vipingamizi
mbalimbali pamoja na kutakiwa kumlipa mwamuzi wa pambano wakati wao
hawakuwa waandaaji.
“Niliwaambia kuwa pambano
limeandaliwa na kampuni inayoiitwa dragon, sasa kwa nini mimi nilipe,
pia niliambiwa nitafute hela ya glovu, niligoma, nadhani hiyo ndiyo
imekuwa chanzo,” alisema Ndambile.
Alisema kuwa ili kumpata mshindi
sahihi, bora pambano hilo lilirudiwe ili mshindi apatikane kwa mujibu wa
taratibu na siyo kwa njia iliyotumika ambayo lengo lake ni kuharibu
rekodi na kutengenza za bondia mwigine.
0 comments:
Post a Comment