KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki
na Kati, Azam FC, ina nafasi nyingine ya kukaa kileleni mwa msimamo wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) endapo itaichapa Lipuli ya
Iringa Jumapili hii, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex saa
1.00 usiku.
Lakini huenda pia ikajihakikishia
nafasi hiyo, kama Mtibwa Sugar iliyokuwa kileleni kwa pointi zake tisa
itapoteza mchezo wake siku hiyo watakapokuwa ugenini kwa mara ya kwanza
msimu huu kuivaa Ruvu Shooting.
Azam FC iliyojikusanyia pointi
saba katika nafasi ya tatu, ikishinda itafikisha pointi 10 na kuiacha
Simba iliyonafasi ya pili kwa pointi zake nane, ambayo ilipata sare ya
mabao 2-2 jana dhidi ya Mbao.
Mabingwa hao waliofanikiwa
kushinda mechi mbili na sare moja, wanaendelea na mazoezi makali kwenye
viunga vyake vya Azam Complex na juzi ilijipima ubavu dhidi ya Friends
Rangers na kuilaza mabao 6-0.
Kocha Mkuu, Aristica Cioaba,
amekuwa akiwapa mbinu mbalimbali wachezaji kuhakikisha wanakuwa imara
kupambana vilivyo na wapinzani wao na kuvuna pointi zote tatu kwa
kushinda kila mchezo.
Azam FC inayodhaminiwa na maji
safi ya Uhai Drinking Water, Benki bora ya NMB na Tradegents, itaingia
dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mechi iliyopita ya ligi kwa
kuichapa Kagera Sugar bao 1-0, lililofungwa na Mbaraka Yusuph.
Lipuli ambayo imejikusanyia jumla
ya pointi tano ikiwa nafasi ya nane kwenye msimamo, imefanikiwa kutoka
suluhu na Ruvu Shooting katika mchezo uliopita, ikiwa ni sare ya pili
msimu huu huku wakiwa wameshinda mchezo mmoja na kutopoteza.
Kihistoria hii itakuwa ni mara ya
kwanza kwa Azam FC kupambana na Lipuli kwenye ligi, lakini itakumbukwa
ya kuwa timu hizo ziliwahi kucheza mchezo wa kirafiki katika maandalizi
ya msimu huu mkoani Iringa na Azam FC kuibuka kidedea kwa ushindi wa
mabao 4-0.
Mabao hayo yaliwekwa kimiani na
beki Yakubu Mohammed, washambuliaji Wazir Junior, Yahya Zayd na kiungo
mng’arisha timu Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambaye amekuwa na kiwango
kizuri cha kufunga mabao kwa misimu hii miwili.
Azam FC inatisha
Mpaka sasa kitakwimu, Azam FC ndio
timu pekee ambayo haijaruhusu wavu wake kuguswa tokea msimu huu uanze
Agosti 26 mwaka huu ikiwa imecheza dakika 270 (sawa na mechi tatu),
ambapo safu ya ulinzi imekuwa ikiongozwa vema na kipa kutoka nchini
Ghana, Razak Abalora aliyepachikwa jina na mashabiki la ‘mikono 100’
kutokana na ubora wake langoni.
Abalora amekuwa akilindwa vilivyo
na mabeki wa kati wenye ubora wa hali ya juu, nahodha msaidizi, Agrey
Moris, Yakubu Mohammed, beki wa kulia Daniel Amoah, wa kushoto Bruce
Kangwa, viungo wakabaji nahodha Himid Mao ‘Ninja’, Stephan Kingue na
Frank Domayo.
Hadi inaingia kwenye mchezo huo,
Azam FC ina majeruhi wawili tu ambao ni wa muda mrefu, winga Joseph
Kimwaga na mshambuliaji Shaaban Idd.
0 comments:
Post a Comment