Wednesday, November 15, 2017

Usiku huu kulikuwa na mechi za mwisho kwa wiki hii za kirafiki kabla ya kurejea katika mechi za vilabu, na timu kubwa za mataifa mbali mbali zilikuwa uwanjani.
Romelu Lukaku ameendelea kufunga na sasa katika mechi mbili za timu ya taifa kwa wiki hii anakuwa amefunga mabao 3 na sasa anakuwa mfungaji bora wa Ubelgiji wa muda wote, ana mabao 31 jumla.
Katika mechi nyingine Mabao mawili ya Alexandre Lacazette yaliibeba Ufaransa na kuwapa sare ya mbili mbili dhidi ya mabingwa wa dunia timu ya taifa ya Ujerumani ambao mabao yao yaliwekwa kimiani na Timo Werner pamoja na Sandro Wagner.
Uholanzi walifanikiwa kuipiga Romania kwa mabao 3 kwa nunge huku mabao ya Uholanzi yakiwekwa kimiani na Memphis Depay, Ryan Babel pamoja na lile la Luuk De Jong.
Timu ya taifa ya Hispania ililazimishwa suluhu ya tatu tatu na waandaaji wa kombe la dunia Urusi huku mabao ya Hispania yakiwekwa kimiani na Jordi Alba na Sergio Ramos (2) na ya Urusi yakifungwa na Fedor Smolov(2) na Alexey Miranchuk.
Nigeria waliishangaza Argentina kwa kutoka nyuma ya bao 2 wakasawazisha na kisha kuibuka kidedea kwa ushindi wa bao 4 kwa 2, Alex Iwobi(2),Kelechi Iheanacho na Brian Idowu walikuwa mashujaa wa Nigeria huku Ever Banega na Sergio Aguero wakiifungia Argentina.
Pale Wembley kulikuwa na mchezo wa kukata na shoka ambapo Brazil walikuwa wageni wa Uingereza katika mchezo ulioisha kwa sare ya bila kufungana.

0 comments:

Post a Comment