Inaelezwa kuwa, Hubert Velud ambaye amezaliwa Juni 8, 1959 mzaliwa wa Vallefranche-sur-Saone nchini Ufaransa, imeripotiwa ametua nchini weekend iliyopita.
Klabu ya Simba bado haijatangaza rasmi kuhusu ujio wa kocha huyo wala haijakanusha taarifa hizo ambazo tayari zimesharipotiwa na baadhi ya vyombo vya habari vya hapa nchini.
Wanasimba wengi wangependa kujua wasifu wa kocha huyo ambaye endapo atatua Simba atakuwa anafundisha soka kwa mara ya kwanza katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.
CV ya Hubert Velud kwa ufupi
Enzi zake wakati anacheza alikuwa golikipa, timu alizowahi kuzicheze ni pamoja na Reims kati ya mwaka 1976 hadi 1989 na Chalons-sur-Marne kati ya mwaka 1989 hadi 1990.
Alianza maisha ya ukocha mwaka 1990 akianza kuifundisha klabu hiyo ya Chalons-sur-Marne ambayo aliitumikia kama mchezaji kabla ya kustaafu. Alifundisha kwa kipindi cha mwaka mmoja tu kuanzia 1990 hadi 1991 kisha kujiunga na Gap ambayo pia alifundisha kwa mwaka mmoja hadi 1992 alipojiunga na Paris FC.
Vilabu vingine alivyowahi kuvifundisha katika nyakati tofauti ni Gazelec Ajaccio, CLermont, Cherbourg, Creteil, Toulon, na Beauvais.
Soka la Afrika
Mwaka 2009 alipenya na kuingia kwenye soka la Afrika kuifundisha timu ya taifa ya Togo (2009-2010), kama unakumbuka ule mkasa wa fainali za AFCON mwaka 2010 kule nchini Angola, alikuwepo kwenye msafara wa kikosi cha Togo kilichoshambuliwa na waasi wa nchi ya Angola, miongoni mwa watu waliojeruhiwa kwenye tukio hilo alikuwa ni Hubert Velud ambaye alipigwa risasi mkononi.
Amewahi pia kuvifundisha vilabu kama Hassania Agadir inayoshiriki ligi kuu ya Morocco (2011-2012), ES Setif (2012-2013), USM Alger (2013-2015), CS Constantine (2015) zote za Algeria, hakudumu sana hapo kabla ya kunyakuliwa na Moise Katumbi kwenda TP Mazermbe baada ya kuwekewa dau kubwa mezani (2016) wakali wa Tunisia Etoile du Sahel wakasikia sifa zake nao wakajitosa (2016-2017).
Mataji aliyowahi kushinda akiwa kocha
Alishinda ligi ya kuu ya Algeria (Ligue Professionnelle 1) mwaka 2013 akiwa kocha wa ES Setif, akiwa hapohapo Algeria mwaka 2013 alifanikiwa kushinda taji la Super Cup akiwa na klabu ya USM Alger baada ya kuachana na ES Setif. Akashinda tena ubingwa wa ligi ya Algeria safari hii akiwa na USM Alger. Alishinda Linafoot na Super Coupe du Congo, huku taji lake kubwa akiwa Afrika ni ubingwa wa Caf Confederation Cup mwaka 2016 akiwa na TP Mazembe.
Kutimuliwa
Mwaka uliopita (2017) alioneshwa mlango wa kutokea na klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia baada ya kushindwa kufuzu hatua ya makundi Caf Champions League.
0 comments:
Post a Comment