Na Zaka Zakazi
Msimu mpya wa Ligi Kuu 2017/18 umeshaanza na leo unaingia katika
raundi yake ya pili. Kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2012/13, Azam FC
imeonodolewa kwenye orodha ya timu zinazopewa nafasi ya ubingwa.
Wachambuzi, mashabiki na hata baadhi ya vyombo vya habari
wanaiangalia Azam FC kama timu itakayopigania kukwepa kushuka daraja
zaidi kuliko kupigania ubingwa. Sababu kubwa ni simulizi zinazoendelea
mtaani kuhusu mabadiliko ya sera za uendeshaji wa timu kutoka kumwaga
mamilioni mpaka kubana matumizi kunakochukuliwa kama sababu ya kuondoka
na wachezaji wake muhimu.
Baada ya kunusurika kushuka daraja katika msimu wake wa kwanza,
2008/09, Azam FC ilijipambanua kama timu ya tajiri mkubwa kwa kuvunja
benki na kukusanya wachezaji nyota.
Mrisho Ngassa alivunja rekodi ya uhamisho kutoka Yanga, Kali Ongala
akarudishwa nyumbani kutoka Sweden na nahodha wa Rwanda, Patrick
Mafisango akashushwa Chamazini, bila kumsahau Peter Ssenyonjo kutoka
Uganda.
Usajili huu ukaibadilisha Azam FC na msimu wake wa pili, 2009/10 na
wa tatu, 2010/11, ikamaliza katika nafasi ya tatu. Baada ya hapo timu
hii ikaanza kupigania ubingwa na misimu miwili mfululizo ya 2011/12 na
2012/13 ilimaliza katika nafasi ya pili. Hatimaye 2013/14 ikachukua
ubingwa!
Azam FC ikaendelea kuwa tishio licha ya kukosa ubingwa mpaka msimu
huu ndipo mitazamo ya watu imebadilika na kuiondoa katika orodha ya
wababe.
Sababu kubwa inawazowaaminisha watu kwamba timu hii itafulia msimu
huu ni kuondoka kwa wachezaji 5 muhimu; Aishi Manula, Shomary Kapombe,
Gadiel Michael, Erasto Nyoni na John Bocco.
MTAZAMO WANGU
-Niliwahi kuongea na Hans van der Pluijm aliporudi Yanga kwa mara ya
pili Disemba 2014 baada ya kuwa aliondoka Juni mwaka huo. Nilimuuliza
kuhusu Yanga aliyoikuta kwa kulinganisha na ile aliyoicha alipoondoka.
Akasema ameumia kutowakuta Kavumbagu, Domayo na Kiiza. Lakini timu ni
kama familia, akifariki mwanafamilia mmoja, mnahuzunika halafu
mnaendelea na maisha. Na yeye atafanya hivyo hivyo.
Ni kweli, Azam FC imeondokewa na wachezaji muhimu kikosini na
kuondoka kwao lazima kutaacha mapengo. Lakini kama alivyosema Hans,
maisha ni lazima yaendelee na katika kufanya hivyo, Azam FC
imesharekebisha baadhi ya mapungufu kwa kuziba mapengo huku mapungufu na
mapengo mengine yakijikebisha yenyewe
i. Aishi Manula
Huyu ni kipa bora misimu miwili iliyopita na amekuwa namba moja wa
Azam FC tangu Machi 19, 2014 kwenye mchezo dhidi ya Yanga uliomalizika
kwa sare ya 1 -1 huku yeye akiokoa penati ya Hamis Kiiza. Aishi pia ni
kipa namba moja wa Taifa Stars. Msimu uliopita ambao ulikuwa wa hovyo
zaidi kwa Azam FC tangu ule wa kwanza wa 2008/09 waliomaliza katika
nafasi ya 8, Aishi alicheza mechi 29 huku mechi 14 akitoka bila kuruhusu
bao. Hizi ni takwimu za kiwango cha juu zinazoweza kukuonesha huyu ni
kipa wa daraja lipi.
Pengo lake lilivyozibwa
Kuondoka kwa Aishi kumewalazimu Azam FC kumsajili kipa namba moja wa
timu ya taifa ya Ghana ya michuano ya Chan, Razak Abalora, kutoka klabu
ya WAFA SC. WAFA SC ni timu inayomilikiwa na akademi ya WAFA(West Africa
Football Academy) iliyopo chini ya klabu ya Feyenoord ya Uholanzi. Hii
ni akademi kubwa kuliko zote Afrika Magharibi.
Mpaka anasajiliwa Azam FC, Razak(20) alikuwa ameshacheza mechi 22 za ligi kuu huku mechi 12 akitoka bila kuruhusu bao.
Kuwa kipa namba moja wa timu ya taifa ya Ghana (japo ni ya CHAN) siyo
kitu cha kubeza hivyo usajili wa kipa huyu unatoa uhakikisho kwamba
nafasi ya Aishi imezibwa vilivyo.
ii. Shomary Kapombe
-Ni ngumu kumpata mtu kama Kapombe kutokana na uzoefu na uwezo wake.
Unapokuwa na Kapombe uwanjani unakuwa na zaidi ya beki wa kulia; ni
kiongozi, ni kiungo na ni mshambuliaji. Mabao yake 8 aliyofunga msimu wa
2015/16, ni ushahidi tosha kuonesha alivyo hatari sehemu zote za
uwanja.
Pengo lake lilivyozibwa
Katika kuziba mapengo ya wachezaji wa aina hii, mara nyingi
kinachohitajika siyo mchezaji mbadala wa sifa za aliyeondoka bali
majukumu wanayopewa uwanjani. Kocha anaweza akabadilisha mbinu ya
uchezaji itakayomfanya atakayechukua nafasi ya aliyeondoka kuyamudu
majukumu bila shida kubwa. Moja ya mbinu hapa huwa kutafuta winga mwenye
asili ya ulinzi ili awe anashuka kumsaidia huyo mbadala.
Kwa Azam FC, upande wa Kapombe yupo Danny Amoah. Huyu jamaa alikuwa
beki wa timu ya Medeama ya Ghana ambayo ilikuwa kundi moja na Yanga robo
fainali ya kombe la shirikisho la Afrika. Yanga walifungwa 3-1 na
Medeama yeye akifunga bao la kwanza. Itakumbukwa kwamba Yanga ile
ilikuwa ya kihistoria. Iliweka rekodi hapa nchini kwa kutwaa ubingwa
ikiwa na pointi nyingi zaidi kuwahi kutokea.
Katika kundi lao, Medeama walimaliza wa tatu kwa pointi zao 8,
wakizidiwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa na waliomaliza katika
nafasi ya pili, Mo Bejaia ya Algeria ambayo ilifika fainali na kufungwa
na TP Mazembe ambayo pia ilikuwa kundi hilo hilo. Medeama ilikuwa timu
pekee kuifunga TP Mazembe kwenye kundi lao. Beki anayetegemewa na timu
ya aina hii siyo wa kuchukuliwa poa.
Lakini pia upande huu yupo Swalehe Abdallah. Kijana huyu aliyetokea
Kahama na kujiunga na akademi ya Azam FC mwaka 2012 sambamba na Aishi
Manula, Ismail Gambo na Braison Rafael, alianzia nafasi za mbele kabla
ya kubadilishwa kuwa beki na kocha wa vijana wakati huo, Vivek Nagul.
Alianza kama beki wa kati na baadaye akawa beki wa kulia.
Bahati mbaya kwake ilikuwa uwepo wa watu watatu kwenye eneo lake,
Erasto Nyoni, Malika Ndeule na Mgaya Abdul(mdogo wa Juma Abdul wa
Yanga).
Kuna wakati alikaribia kwenda Yanga lakini sijui nini kilitokea,
akaenda Stand Utd halafu Majimaji. Msimu huu, baada ya Azam FC kushindwa
kumpata Salum Kimenya wa TZ Prisons, wakaamua kumrudisha kijana wao
huyu Chamazini.
Uzoefu wake wa kucheza mbele ambako ndiko alikoanzia, na beki wa kati
aliporudi nyuma, vinaweza kumsaidia kuyamudu majukumu mapya ndani ya
kikosi cha Azam FC. Kumbuka bao alilofunga dhidi ya Onduparaka FC kule
Uganda kwenye pre season, ni la kiwango cha mshambuliaji mzoefu, siyo
beki…ni kama alivyokuwa akifanya Kapombe.
3. Gadiel Michael
Ni mmoja wa wachezaji wa akademi aliyetoa mchango mkubwa kwenye msimu
wa ‘unbetean run’ ambao Azam FC walichukua ubingwa bila kupoteza mchezo
hata mmoja na kuingia katika vikosi vya ‘Invicibles’. Gadiel pia ni
beki tegemeo kwa sasa katika timu ya taifa, Taifa Stars.
Pengo lake lilivyozibwa
Katika wachezaji muhimu wa Azam FC waliondoka msimu huu, Gadiel ni
mchezaji aliyekuwa na umuhimu mdogo zaidi. Nafasi yake haihitaji nguvu
nyingi kuiziba kwa sababu hakuwa mchezaji wa kuweza kutegemewa msimu
mzima. Gadiel ni mchezaji asiye na ‘consinstence’ yaani muendelezo wa
kiwango. Mara zote amekuwa na homa za vipindi.
Kuna wakati huwa anakuwa kwenye ‘fomu’ ya hali ya juu halafu anashuka
mpaka kiwango cha chini kabisa. Katika kipindi chake chote cha ‘maji
kupwa maji kujaa’, nafasi yake ilikuwa chini ya ‘kiraka’ Erasto Nyoni.
Hii ikaendelea mpaka akasajiliwa Bruce Kangwa kutoka Zimbabwe. Kangwa,
mchezaji aliyekuwa kwenye kikosi cha Zimbabwe kilichoshiriki AFCON 2017,
ni wa daraja la juu zaidi kuliko Gadiel. Ila kwa kuwa tayari Gadiel
alikuwepo wakati ule, na Kangwa alikuwa na uwezo wa kucheza kama winga
tangu akiwa kwao, akaanza kwa kutumika mbele, lakini kwa sasa atarudi
chini na kumfanya Gadiel asaulike kabisa. Nafasi atakayoiacha kule mbele
kushoto itazibwa na Enoch Atta Agyei ambaye msimu huu ataitumikia Azam
FC baada ya kubanwa na kanuni hapo kabla licha ya kusaijiliwa tangu
2016.
4. Erasto Nyoni
Kwa sasa hapa nchini hakuna mchezaji kiraka kama Erasto Nyoni. Huyu
jamaa anacheza karibu nafasi zote kasoro kudaka tu. Kwa kifupi, Erasto
ni ‘most complete technical player’ hapa nchini. Anaweza akaingia kwa
ajili ya kuifanya kazi moja tu, kumpoteza ‘mtu hatari’ uwanjani.
Kocha wa sasa wa Man U, Jose Mourinho, alikuwa na msemo wake wakati
akiwa Chelsea katika awamu yake ya kwanza, ‘make it 10 against 10’,
yaani kuifanya mechi kuwa ya wachezaji 10 kwa 10. Kama wapinzani
walikuwa na mchezaji hatari, alikuwa anamtuma Geremi Njitap kwenda
kumpoteza na kupotea naye. Hapo anakuwa ameifanya mechi iwe ya wachezaji
10 kwa 10 badala ya 11 kwa 11. Geremi akiingia, anampoteza mtu na yeye
anapotea…waliobaki ndiyo wanaocheza, na Erasto pia kazi hii anaiweza kwa
uzuri wa kutosha.
Pengo lake linavyozibwa.
Licha ya ubora wote huo wa Erasto, ni vigumu kumuona kama mchezaji
muhimu kwenye timu kwa sababu hana namba maalumu atakayoacha pengo. Yeye
amekuwa akitumika kuziba mapengo ya wengine kwa hiyo wenyewe wakiwepo,
yeye haonekani muhimu. Hii ni sehemu moja na kubwa sana ya mchezaji kama
huyu kutoacha pengo anapoondoka.
5. John Bocco
Hakuna ubishi kwamba huyu jamaa alikuwa muhimu zaidi kwa Azam FC
kuliko wengine wote walioondoka. Siyo kwa sababu ya historia yake bali
mchango aliokuwa akiendelea kuutoa ndani na nje ya uwanja.
Wachezaji wenzake walikuwa wanamuita Mr. Azam FC na uwepo wake
ulikuwa muhimu kila wakati. Mwaka 2016, Azam FC walitoka sare ya 2-2 na
JKT Ruvu. Azam waliongoza 2-0 kipindi cha kwanza lakini zikarudi zote
kipindi cha pili. Baada ya mchezo huu, John Bocco alibaki peke yake
kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, akilia kwa uchungu. Matokeo
yalimuumiza sana. Matukio kama haya kwa Bocco ni mengi mno kwa sababu
aliamini Azam FC ni sehemu ya damu yake.
Lakini vitu vizuri vyote hufikia wakati vinaisha na hivyo hivyo kwa nyakati nzuri za John Bocco Azam FC zikafikia mwisho.
Pengo linavyozibwa
Tangu alipokuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu wa 2011/12, Bocco
amekuwa kinara wa mabao kwa Azam FC kila msimu kasoro mmoja tu, 2012/13
ambapo pacha wake Kipre Tchetche alimzidi klabuni na kwenye ligi kwa
ujumla.
Kuziba pengo la mtu kama huyu haiwezekani hata kidogo. Arsenal
hawatakuja kuziba pengo la Henry, Barcelona hawatakuja kuziba pengo la
Messi. Ila kwa kuwa maisha ni lazima yaendelee, Azam FC imesajili
washambuliaji kadhaa wanaoweza kuleta mabao Chamazini.
i. Mbaraka Yusuph
-Mabao yake 12 msimu uliopita yanatoa ishara kwamba Azam FC wanaweza
kufaidika naye katika maisha yao mapya. Zaidi ya kufunga tu, Yusuph pia
ni mzuri kwenye kuumiliki na kuudhibiti mpira, anaweza kuwahadaa mabeki
na anapiga kwa miguu yote. Akifunga kuanzia mabao 7 atakuwa amepunguza
machungu ya kumkosa Bocco kwa kiasi fulani.
ii. Waziri Junior
-Alimaliza msimu uliopita kwa mabao 7 akiwa na timu yenye viungo
wanaotoa msaada hafifu Toto Africans. Endapo atatulia na kuweka akili
zake kwenye kuzipasia nyavu za wapinzani, huku akipata msaada kwa viungo
wenye uwezo mkubwa kuliko aliocheza nao msimu ulipoita anaweza
akasaidia kupunguza mzigo wa majonzi ya kuondoka kwa Bocco.
iii. Yahaya Zayd
Ni wonder kid aliyeibuka kutoka akademi, kule kule walikotoka wakina Aishi Manula na Gadiel Michael.
Msimu uliopita alipelekwa kwa mkopo Ashanti United alikofunga mabao 9 ligi daraja la kwanza.
Kwenye mechi za kujiandaa na msimu mpya, amefunga takribani mabao 5,
kuanzia Iringa dhidi ya Lipuli mpaka Uganda. Kama ataifungia Azam FC
mabao kuanzia 5 kwenye ligi kuu, utakuwa msaada mkubwa sana kwao.
Washambuliaji hawa wakisaidiana na waliokuwepo hapo kabla, wanaweza kuisaidia pakubwa sana klabu hii
i. Shaban Idd Chilunda
alifunga mabao 7 msimu uliopita na kuwa mfungaji bora namba mbili wa
klabu, mabao 2 nyuma ya John Bocco. Alianza kupata nafasi ya uhakika
mzunguko wa pili wa ligi baada ya kuumia John Bocco kwenye mchezo dhidi
ya Simba SC Januari 28 ambapo Bocco mwenyewe alifunga bao la ushindi.
Msimu huu anaweza kufanya kitu kikubwa zaidi kutokana na angalau kuizoea
ligi kidogo.
ii. Yahaya Mohamed
Huyu ni mfungaji bora wa ligi ya Ghana msimu wa 2016. Alimaliza akiwa na
mabao 16. Bahati mbaya kwake ni kwamba mambo hayakumuendea vizuri
Tanzania katika msimu wake wa kwanza. Matokeo yake hata yeye mwenyewe
akaanza kutilia shaka uwezo wake, hapo ndipo alipopotea.
Msimu huu anaonekana kuanza vizuri, mabao yake matatu aliyoyafunga
Uganda kwenye pre season na moja la ufunguzi wa msimu dhidi ya Ndanda
FC, yanaweza kumjenga kisaikolojia kwa kiwango kikubwa na kumrudishia
kujiamini kwake kulikopotea msimu uliopita.
Kikubwa ambacho watu wengi hawakiangalii aidha kwa makusudi au bahati
mbaya kwa Azam FC ni kwamba timu hii ilikuwa na kikosi kipana chenye
wachezaji wawili mpaka watatu kwenye namba moja, tena wa kiwango cha juu
sana. Tatizo ni kwamba huwezi kupanga wachezaji 13 uwanjani hivyo
wengine wakawa wanakosa nafasi kwa sababu walimu huwa na tabia ya
kukariri wachezaji.
Kila jambo zuri huwa na upande wa pili ambao huwa siyo mzuri, hali
kadhalika kwa jambo baya, nalo huwa lina upande wake wa pili ambao huwa
ni mzuri. Kuondoka kwa walioondoka ndani ya Azam FC ni jambo baya lakini
lina upande wake wa pili ambao ni mzuri.
i. Kunapunguza presha.
Azam FC imekuwa ikihesabiwa kama timu ya ubingwa kwa misimu mitano sasa.
Hii iliwaongezea presha wao wenyewe kutaka kuthibitisha heshima
waliokuwa wakipewa. Ikitokea wakakosa matokeo, wanaharibikiwa vichwa.
Pia ilisababisha mechi zao zote ziwe ngumu sana kwa sababu wapinzani wao
walijiandaa kucheza na timu yenye hadhi ya bingwa.
Kwa sasa presha hii haipo tena kwa sababu ule mzigo wameutua. Timu
zinaweza kuingia uwanjani dhidi ya Azam FC zikijiamini zinakwenda
kucheza na kibonde mwenzao. Hii ndiyo iliyoisaidia Leicester City kuwa
bingwa 2016.
ii. Nafasi kwa wengine
Kuondoka kwa waliondoka kunakunatoa mwanya kwa waliokuwa wakikosa
nafasi, kutoa mchango wao. Pia maeneo muhimu ya timu, kama kiungo na
safu ya ulinzi, kwa asilimia kubwa imebaki na watu wale wale.
i. Yakub Mohamed
ii. Aggrey Moris
iii. Himid Mao
iv. Sure Boy
v. Kingue Mpondo
Hawa ni mihimili ya Azam FC na bado wapo kwenye timu. Lakini hayo yote yataanza na mechi ya leo.
Ni mechi ya kudhihirisha au kupotea kwa Azam FC.
Home
»
»Unlabelled
» Ni mechi ya kudhihirisha au kupotea kwa Azam FC
Saturday, September 9, 2017
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment