Saturday, January 13, 2018


TIMU ya Mtibwa Sugar ya Morogoro imepanda hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Lipuli Uwanja wa Samora mjini Iringa leo.
Shukrani kwa mfungaji wa bao hilo, kiungo Hassan Dilunga aliyefunga dakika ya 37 na sasa Mtibwa Sugar inafikisha pointi  24 baada ya kucheza mechi 13, ikizidiwa kwa pointi mbili mbili na Simba na Azam FC na ikiwazidi kwa pointi tatu mabingwa watetezi, Yanga.
Zote, Azam, Simba na Yanga zitacheza viporo vyao vya Raundi ya 13 mapema wiki ijayo sawa na Singida United ambayo sasa inashika nafasi ya nne kwa pointi zake 23.
Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Stand United imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting bao pekee la : Bigiramana Babibakuhe dakika ya 47 Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, wakati Ndanda FC imelazimishwa sare ya 1-1 na Mbao FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
Emmanuel Mvuyekure alitangulia kuifungia Mbao FC dakika ya 32, kabla ya Nassor Kapama kuwasawazishia wenyeji dakika ya 65.
Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi ya mahasimu wa Jiji la Mbeya, Tanzania Prisons na Mbeya City Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya wakati Janauri 15, Njombe Mji wataikaribisha Kagera Sugar FC Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe na Janauri Yanga SC watakuwa wenyeji wa Mwadui FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mzunguko wa 13 utahitimishwa kwa michezo miwili Januri 18, Simba wakiikaribisha Singida United Uwanja wa Taifa na Maji Maji wakiwa wenyeji wa Azam FC Uwanja wa Maji Maji mjini Songea.

0 comments:

Post a Comment