Thursday, February 1, 2018







WAKATI timu ikijiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting kutoka Pwani, utakaopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, amesema wanahitaji kupata ushindi ili kuwaongezea ari wachezaji wao kuelekea mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.


Akizungumza na gazeti la Nipashe jana jijini Dar es Salaam, Djuma, ambaye timu yao inadhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, alisema kuwa timu inayoshinda inakuwa imara katika mchezo unaofuata na uwezo wa kujiamini wa wachezaji wake unaongezeka.

Djuma alisema wanaendelea na mazoezi kila siku kwa sababu wanataka kuona wanapata pointi tatu katika kila mchezo wanaocheza hatua ya lala salama ambayo bingwa wa Ligi Kuu Bara hupatikana.

"Tunajua tuko mbele na wenzetu wanatuangalia ili watufikie, tumejipanga kuwakimbia na hili litafanikiwa kwa sisi kuendelea kushinda, kufanya vizuri kwenye ligi ya Tanzania, kutatuweka vizuri pia kwenye mashindano ya CAF (Kombe la Shirikisho Afrika)," alisema kocha huyo raia wa Burundi.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, alisema jana kuwa mchezo kati ya Simba na Azam FC unaotarajiwa kufanyika Februari 7, mwaka huu, utafanyika kama ulivyopangwa na ule wa ugenini dhidi ya Mwadui FC umesogezwa mbele.

Baada ya mchezo dhidi ya mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, vinara hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara watajiandaa kuwakaribisha Gendarmarie Nationale katika mchezo wa kwanza wa raundi ya awali ya mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho.

Simba ndio vinara wa ligi wakiwa wamejikusanyia pointi 35 na ni timu pekee ambayo haijafungwa katika mechi za mzunguko wa kwanza wakifuatiwa na Azam FC wenye pointi 30, mabingwa watetezi, Yanga wao wana pointi 28 na Singida United yenye pointi 27 wako katika nafasi ya nne kwenye msimamo.

Wekundu wa Msimbazi watashuka uwanjani pia wakiwa na kumbukumbu ya ushindi katika mechi zake nne zilizopita ambazo ilipata pointi 12 na mabao 12 ya kufunga huku pia wakikumbuka kichapo cha mabao 7-0 walichoipa Ruvu Shooting kwenye mchezo wa kwanza msimu huu.

0 comments:

Post a Comment