Friday, May 11, 2018

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Tanzania inaendelea vizuri na maandalizi ya michuano ya soka ya Mataifa ya Afrika kwa vijana wa chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U17) yanayotarajiwa kufanyika nchini mwakani.Ametoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma leo alipojibu swali la Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM) wakati wa kipindi cha 'Maswali kwa Waziri Mkuu'.
Katika kujenga hoja yake kabla ya kuuliza swali, Ndassa amesema Tanzania imepewa heshima kubwa ya kuandaa mashindano hayo hivyo ni vyema ikajiandaa vizuri kupokea wageni.
“Serikali imejipangaje kufanikisha mashindano hayo?" mbunge huyo kutoka Mwanza amehoji.
Waziri Mkuu, Dk. Kassim Majaliwa maandalizi ya AFCON U17  yanaendelea vizuri 

Akimjibu mbunge huyo, Waziri Mkuu amesema maandalizi kwa ajili ya mashindano hayo yanaendelea.
“Niwahakikishie watanzania, maandalizi juu ya mashindano yetu yote yanaendelea kama kawaida. Nitoe wito kwa watanzania tuendelee kuziunga mkono hasa timu zote zinazofikia mashindano ya kimataifa ili ziweze kufanya vizuri," amesema.
“Kwa ujumla, timu hizi zote (za vijana) ambazo tunazo katika ngazi ya kimataifa ni jukumu letu kuziandaa na mimi naishukuru TFF (Shirikisho la Soka) pamoja na maandalizi kwa sasa yanaendelea na ninazo taarifa moja ya maandalizi hayo ni timu yetu kwenda Sweden kujiandaa kwa ajili ya mashindano hayo.
“Sambamba na hayo] tunajianda kwa viwanja vitakavyochezewa, maeneo ambayo yatafikiwa na wageni kwa sababu kutakuwa na wageni wengi na mambo yote ambayo yanahusiana na afya pamoja na usafiri wao."
Baada ya majibu hayo, Ndassa akasimama na kuuliza swali la nyongeza akihoji serikali itavitangazaje vivutio vyake kutokana na wageni wengi kuja nchini kuangalia mashindano hayo.
“Kupitia mashindano hayo, kwa sababu kutakuwa na wageni wengi kutoka nje, kwa sababu tunazo  fursa za utalii, je, Tanapa (Shirika la Hifadhi za Taifa) na Ngorongoro watashirikishwa kwa namna gani ili kuvitangaza vivutio vilivyopo nchini?” Ndassa amehoji.
Katika majibu yake kwa mbunge huyo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema: “Mipango ambayo Wizara ya Maliasili na Utalii inayo ni kuimarisha sekta ya utalii kwa kutangaza mapori na maeneo yote nchini.
“Tutawapeleka Kilwa wakaone majengo ya zamani yaliyokaliwa na Waarabu na maeneo mengine na nafasi hii tutaitumia vizuri."

0 comments:

Post a Comment