Kamati ya Tuzo za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL),
imekamilisha uteuzi wa wachezaji 3 watakaowania tuzo ya mchezaji bora wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2017/2018.
Wachezaji watatu waliobaki katika kinyang’anyiro hicho
ni Emmanuel Okwi, John Bocco na Erasto Nyoni wote wa Simba, ambapo
kamati ya Tuzo hiyo ya Mchezaji Bora imeandaa utaratibu wa kupiga kura
kuwashirikisha Wahariri wa Habari za Michezo, manahodha wa timu za Ligi
Kuu ya Vodacom na makocha wa timu za Ligi Kuu.
Pia kamati imekamilisha uteuzi wa wachezaji watakaowania
tuzo katika kategori mbalimbali kwenye sherehe hizo za Tuzo ya Mchezaji
Bora wa VPL itakayofanyika ukumbi wa Mlimani, City Dares Salaam Juni 23
mwaka huu.
Tuzo 16 zinatarajiwa kutolewa siku hiyo, ambapo baadhi
ni za kikanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara, ambazo tayari washindi wake
wamefahamika, ambazo ni bingwa, mshindi wa pili, mshindi wa tatu,
mshindi wa nne na mfungaji bora.
Ukiacha hizo tano za kikanuni, zipo tuzo 10 ambazo
zimefanyiwa kazi na Kamati ya Tuzo kulingana na takwimu mbalimbali za
ligi hiyo, ambapo tuzo moja nyingine ya Mchezaji Bora chini ya umri wa
miaka 20 (Tuzo ya Ismail Khalfan), inayohusisha vikosi vya vijana vya
timu za Ligi Kuu yenyewe inaendelea kufanyiwa kazi kwa vile mashindano
yanaendelea mkoani Dodoma na itakapokamilika watatangazwa wateule
watatu.
Tuzo nyingine zitakazotolewa siku hiyo ni Timu yenye
Nidhamu inayowaniwa na Kagera Sugar, Simba na Mtibwa Sugar, wakati
Mchezaji Bora Chipukizi inawaniwa na Shaaban Idd Chilunda, Yahya Zayd
(Azam) na Habibu Kiyombo (Mbao).
Mwamuzi Msaidizi Bora inawaniwa na Helen Mduma, Mohammed
Mkono na Ferdinand Chacha, wakati Mwamuzi Bora wateule ni Elly Sasii,
Jonesia Rukyaa na Hans Mabena.
Tuzo ya Kipa Bora wanaowania ni Aron Kalambo (Prisons),
Aishi Manula (Simba) na Razack Abalora (Azam), huku Kocha Bora wateule
ni Abdallah Mohamed (Prisons), Zuberi Katwila (Mtibwa) na Pierre
Lechantre (Simba), goli Bora ni Seif Karihe (Lipuli) na Shaaban Idd
Chilunda (Azam) ambaye ameingiza mabao mawili.
Tuzo nyingine ambazo zitatolewa Juni 23 ni Mchezaji wa
Heshima ambayo licha ya kuwa kamati ina majina ya wachezaji mbalimbali
inaoona wanastahili tuzo kwa mwaka husika, lakini haitangazi majina
hayo, isipokuwa hutaja jina la aliyepewa tuzo siku ya sherehe na pia
kitatangazwa kikosi bora cha msimu.
IMETOLEWA NA TFF
0 comments:
Post a Comment