Saturday, August 18, 2018


MWENYEKITI mstaafu wa klabu ya Yanga SC, Yussuf Manji atakuwepo Uwanja wa Taifa Jumapili wakati wa mchezo wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika baina ya timu yake hiyo na U.S.M. Alger ya Algeria.
Taarifa ya Yanga SC leo imesema kwamba mgeni rasmi katika mchezo huo atakuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (JWTZ), Jenerali Venance Mabeyo na kwamba Manji pia atakuwapo.
Manji alijiuzulu Uenyekiti wa Yanga SC Mei mwaka jana, lakini mkutano wa wanachama wa Juni 10 mwaka huu ulimkatalia ombi hilo, ingawa tangu wakati huo amekuwa kimya.  

Yussuf Manji atakuwepo Uwanja wa Taifa Jumapili Yanga ikimenyana na U.S.M. Alger ya Algeria

Kikosi cha Yanga bado kipo Morogoro na sasa kitarejea mapema kesho kwa maandalizi ya mwisho ya mchezo huo, ambao viingilio vitakuwa Sh. 3,000 mzunguko, Sh. 7,000 VIP B na C watalipa na Sh.10,000 VIP A.
Mchezo huo utachezeshwa na Jackson Pavaza atakayepuliza filimbi akisaidiwa Matheus Kanyanga na David Tauhulupo Shaanika wote kutoka Namibia.
Yanga SC ambayo itajaribu kusaka ushindi wa kwanza katika mechi zake za Kundi D Jumapili baada ya sare moja na kufungwa mechi tatu za awali, inatarajiwa kuwasili kesho kutoka Morogoro ilipokuwa imeweka kambi kwa wiki mbili.
Yanga SC Ilianza michuano hiyo kwa kuchapwa mabao 4-0 na U.S.M. Alger nchini Algeria kabla ya kuja kutoa sare ya 0-0 na Rayon mjini Dar es Salaam na baadaye kwenda kufungwa mfululizo na Gor Mahia, 4-0 nchini Kenya na 3-2 Tanzania.
Mchezo wa Jumapili safu ya ushambuliaji ya Yanga itaongezewa nguvu na mshambuliaji mpya, Heritier Makambo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambaye amepatiwa leseni na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Kocha Mkongo wa Yanga, Mwinyi Zahera anatarajiwa kuwa kwenye benchi la timu kwa mara ya kwanza tangu aajiriwe miezi miwili iliyopita.

0 comments:

Post a Comment