Bondia
wa ngumi za kulipwa nchini, Mada Maugo wa Tanzania amemchapa kwa
pointi, mpinzani wake, Charles Misanjo wa Malawi katika pambano la
kimataifa la uzito wa Super Middleweight kwenye ukumbi wa PTA jijini.
Wakati
Maugo anashinda kwa pointi, bondia nyota nchini,Ibrahim Class
alidhihirisha ubora wake baada ya kushinda kwa Technical knockout (TKO)
raundi ya tano katika uzito wa Super Feather.
Pambano
hayo yaliandaliwa kwa lengo la kutafuta mataulo ya kike kwa wanafunzi
wa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kwa kushirikiana na taasisi ya
She Can Foundation.
Katika
pambano hilo lililoandaliwa na promota wa kwanza wa kike nchini, Sophia
Mwakagenda wa kampuni ya Lady In Red Promotion, Maugo alipata pointi
77-75 kutoka kwa jaji, Mwinyi Milla, 78-74 (Modesti Rashid) na 76-76
kutoka kwa jaji, Chaurembo Palasa.
Pamoja
na ushindi huo ulilalamikiwa na Misanjo na baadhi ya mashabiki wa ngumi
za kulipwa, Maugo alisema kuwa Mmalawi alikuwa anapiga makofi baadala
ya ngumi ndiyo maana ameonekana kushambulia sana.
“Mimi
nimekuwa nikipigana kwa kutafuta pointi kwa kupiga ngumi, yeye alikuwa
anapiga makofi muda wote na kusukuma, hao mashabiki na bondia inaonekana
hawajui ngumi, sijapendelewa kwa sababu ya Utanzania, hapana,” alisema
Maugo.
Misanjo
alisema kuwa haikuwa ngumi za kawaidi bali ni vita. “Matokeo
sikubaliani nayo, yanaua mchezo wa ngumi za kulipwa nchini Tanzania,
itatufanya tusiwe tunakuja kupigana kutokana na maamuzi kama haya,”
alisema Misanjo.
Pambano
kati ya Ibrahim Class na Baina Mazola ndilo lilikuwa na msisimko mkubwa
ambapo mabondia hao walionyesha uwezo mkubwa. Class alianza pambano kwa
kasi na kutawala raundi mbili za mwanzoni huku Mazola alikitawala
raundi ya tatu.
Mabondia
hao walipigana kwa visasi na kuleta burudani ya aina yake. Class
alionekana kutumia uzoefu zaidi na kufanikiwa kumchana jicho Mazola
katika dakika ya 1.47 ya raundi ya tano na kuibuka mshindi.
“Nimepoteza
kwa kuumia, hata hivyo nitamtafuta tena Class ili kuonyesha kuwa mimi
ni bora zaidi yake,” alisema Mazola. Class alisema kuwa mpinzani wake ni
mzuri na ushindi ni jambo la kawaida sana kwake.
“Mimi ni bondia bora, hilo halina ubishi,Mazola bado sana kwangu, afanyekazi ya zaida kunifikia na kunishinda,” alitamba Class.
Bondia
Flora Machela alifanikiwa kushinda kwa TKO raundi ya tano dhidi ya
Sarafina Julius katika pambano la uzito wa bantam wakati Asha Ngedere na
Happy Daudi wakitoka sare kwa katika pambano la uzito wa Super Light.
Akizungumza
baada ya pambano hilo, promota Mwakagenda aliwapongeza wadau na
makampuni yaliyochangia kufanikisha tukio hilo japo lengo la kukusanya
mataulo 40,000 halijafanikiwa.
“Huu
ni mwanzo na jambo hili ni geni kwangu, ndiyo kwanza nimeandaa ngumi za
kulipwa na nimeona changamoto zake, nimejifunza na nitaendelea kuandaa
kwa malengo maalum,” alisema Mwakagenda.
0 comments:
Post a Comment