MSHAMBULIAJI David Molinga wengi wanapenda kumuita mwili jumba ama Falcao raia wa DR Congo guu lake la kulia limekwama Uwanja wa CCM Kirumba kwa muda wa dakika 315.
Nyota huyo tangu afunge bao lake la mwisho uwanjani hapo dhidi ya Alliance Novemba 29, 2019 wakati Yanga iliposhinda 2-1, hajafunga tena hadi sasa, zikiwa zimepita mechi nne huku yeye akicheza dakika 315 katika mechi hizo bila bao.
Molinga mwenye mabao manne kwa sasa, alianza kwa kasi ya kutupia huku akipata umaarufu kwa kutumia zaidi guu la kulia kufunga mabao ya moja kwa moja akiwa nayo mawili mpaka sasa.
Alianza kufunga bao lake la kwanza kwenye mchezo wa pili wa Yanga dhidi ya Polisi Tanzania kwenye sare ya mabao 3-3, ambapo alifunga dakika ya 64 kwa kichwa akimalizia pasi ya Mrisho Ngassa na la pili alifunga kwa faulo dakika ya 68 kwa guu lake la kulia.
Bao la tatu alifunga mbele ya JKT Tanzania kwa faulo dakika ya 34, baada ya Deus Kaseke kuchezewa rafu na Yanga ilishinda mabao 3-2 dhidi ya JKT Tanzania mechi zote zilichezwa Uwanja wa Uhuru.
Mara ya mwisho kufunga bao lake la nne ilikuwa Uwanja wa CCM Kirumba ambapo guu lake la kulia lilicheka na nyavu dakika ya 71 akimalizia pasi ya Deus Kaseke kwenye ushindi wa mabao 2-1 na hakuweza kufurukuta kwenye mechi nne za Yanga zilizofuata, ambazo alicheza kwa dakika 315.
Dakika hizo zinatimia kwani kwenye mchezo wake wa nne wakati Yanga ikishinda bao 1-0 dhidi ya Biashara United alicheza dakika 45, nafasi yake ilichukuliwa na Tariq Seif Uwanja wa Taifa.
0 comments:
Post a Comment