WAKATI
mashabiki wa soka hapa nchini wakiendelea kupishana kauli juu ya
mshambuliaji wa Simba, Mnyarwanda, Meddie Kagere kuwa alikuwa na hirizi
uwanjani katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga huku wengine
wakipinga, Championi Jumatano limepata ukweli wa jambo hilo.
Simba na Yanga zilicheza
Jumamosi iliyopita kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara ambapo timu hizo
zilitoka sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa Taifa.
Katika
mitaa mbalimbali hapa nchini jambo hilo limekuwa gumzo kubwa lakini
kila mtu amekuwa akisema la kwake bila ya kuwa na ukweli wowote.
Hata
hivyo, kutokana na hali hiyo mmoja wa waamuzi waliochezesha mechi hiyo
iliyokuwa na ushindani mkubwa, ameliambia gazeti hili kuwa, Kagere
hakuwa na hirizi katika mchezo huo kama wengi wanavyofikiria.
“Watu wengi tumetawaliwa sana na mawazo ya ajabu na yasiyokuwa na faida yoyote katika maendeleo ya soka letu.
“Kagere
hakuwa na hirizi katika mchezo huo bali ile ilikuwa ni cheni ambayo
aliokota uwanjani na kumpatia mwamuzi Jonesia Rukyaa ambaye pia
aliipeleka kwa mwamuzi wa akiba naye akaipeleka katika benchi la ufundi
la Simba.
“Kwa hiyo,
hao wanaosema kuwa Kagere alikuwa na hirizi katika mchezo huo ni
waongo, niwaombe tu wasiwe wepesi wa kusema vitu wasivyokuwa na uhakika
navyo, hata kama utamuuliza Rukyaa naye atakwambia hivyo hivyo, japokuwa
maadili hayaturuhusu kusema chochote kabla ripoti zetu kufanyiwa kazi
na TFF,” alisema mwamuzi huyo kwa sharti la kutotajwa jina lake
gazetini.

0 comments:
Post a Comment