Thursday, January 2, 2020


HATIMAYE kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima amewasili leo mchana kujiunga tena na klabu ya Yanga akitokea AS Kigali ya kwao.
Haruna alipokewa na Maafisa wa Yanga, wakiwemo Mhamasishaji na Msemaji, Antonio Nugaz na Afisa Habari, Hassan Bumbuli Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kabla ya kupelekwa kambini, hoteli ya Protea, Masaki kuungana na wenzake.
Haruna amesajiliwa tena Yanga SC dirisha dogo, mwezi huu baada ya misimu miwili ya kuwatumikia mahasimu wa jadi, Simba SC kabla ya kwenda kucheza kwa nusu msimu AS Kigali.

Haruna Niyonzima akiwa na Afisa Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz baada ya kuwasili JNIA leo 

Haruna ambaye Februari 5 atatimiza miaka 30 ya kuzaliwa, alijiunga na Yanga SC kwa mara ya kwanza mwaka 2011 akitokea APR ya kwao, baada ya awali kuchezea Etincelles kuanzia 2005 hadi 2006 alipohamia Rayon Sports alikocheza kwa msimu mmoja pia.
Amekuja nchini siku mbili kabla ya mchezo mkali dhidi ya mahasimu wa jadi, Simba SC utakaofanyika Jumamosi Uwanja wa Taifa na viongozi wanajaribu kukamilisha taratibu ili ashiriki mechi hiyo.
Anakuwa mchezaji mpya wa tano kusajiliwa Yanga SC dirisha dogo baada ya beki Adeyoum Ahmed na washambuliaji Ditram Adrian Nchimbi, Tarek Seif Kiakala na Muivory Coast, Yikpe Gilslain Gnamien.
Na hiyo ni baada ya kuachwa kwa washambuliaji wawili, Mganda Juma Balinya na Mnamibia, Sadney Urikhob ambao wote walisajiliwa mwanzoni mwa msimu.
Wakati huo huo, Yanga SC imemteua mchezaji wake wa zamani, Abeid Mziba ‘Tekero’ kuwa Meneja mpya wa timu baada ya kumsimamisha Dismas Ten aliyekuwa anakaimu nafasi hiyo kufuatia kuondolewa kwa Hafidh Saleh. 
Mziba alikuwa mshambuliaji tegemeo Yanga SC miaka ya 1980 kabla ya kufanya kazi kama Kocha Msaidizi wa Raoul Shungu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

0 comments:

Post a Comment