Na Saleh Ally
MTANZANIA
Mbwana Samatta amefanikiwa kucheza mechi mbili tu katika kikosi cha
Aston Villa ya England lakini tayari ni maarufu sana.
Samatta
amecheza mechi moja ya Carabao Cup dhidi ya Leicester City na
wamefanikiwa kufika fainali, sasa watakutana na Manchester City jambo
linalosubiriwa kwa hamu sana.
Mechi
ya pili ilikuwa ni ya Premier LEague, Samatta akiweka rekodi ya kuwa
Mtanzania wa kwanza kucheza ligi hiyo. Kama haitoshi, katika mechi ya
kwanza akafanikiwa kufunga bao lake la kwanza licha ya kuwa walipoteza
kwa mabao 2-1.
Mambo
haya yamechangia kumfanya awe maarufu kwa mashabiki wa Aston Villa
ingawa lile la mashabiki wengi wa Tanzania kuvamia mitandao nalo
lilichangia.
Kuendelea
kuifahamu vizuri Aston Villa ambayo yuko Samatta ni vizuri zaidi na
mmiliki wake, anatokea Afrika kwa maana ya nchini Misri.
Nassef Sawiris ndiye tunayemzungumzia. Mmiliki wa timu hiyo ya England ambayo ni moja ya timu kongwe katika soka la England.
Ingawa
si maarufu sana Tanzania, nchi nyingi duniani amekuwa maarufu kutokana
na utajiri wake pia akijihusisha na mambo kadhaa yakiwemo ya michezo.
Unapowataja
watu kadhaa maarufu hasa matajiri katika soka kama Roman Abramovich,
mmiliki wa Chelsea au Sheikh Mansour anayeimiliki Manchester City,
karibu kila mpenda soka anawafahamu lakini kwa Tanzania Sawiris si sana.
Pamoja
na hivyo, katika orodha ya matajiri wanaomiliki timu za England, kwa
utajiri Sawiris anashika namba tano baada ya Sheikh Mansour anayeongoza
akiwa na utajiri wa dola bilioni 30 akitokea katika familia ya kifalme
ya Abu Dhabi.
Abramovich
anafuatia akiwa na dola bilioni 12.4, nafasi ya tatu ni mmiliki wa
Arsenal FC, huyu ni Mmarekani Stan Kroenke mwenye utajiri wa dola
bilioni 8.7 na nafasi ya nne ni mmiliki wa Klabu ya Wolverhampton,
anaitwa Guo Guangchang, utajiri wake ni dola bilioni 6.7.
Sawiris
mwenye utajiri wa dola bilioni 6.4, anafunga tano bora ya matajiri
wanaomiliki timu za Ligi Kuu England kwa maana ya utajiri wao.
Wakati
Sheikh Mansouri ana rekodi ya utajiri ya dola milioni 82.7 kumsajili
Kevin De Bruyne kutoka Wolfsburg, Sawiris naye amejitutumua kwa kuwa na
rekodi ya kutoa dola milioni 27.2 kumsajili Wesley kutoka Club Brugge ya
Ubelgiji. Mshambuliaji huyu ndiye aliyeumia na kusababisha Samatta
kutua Genk.
Sawiris
ni namba nne kwa utajiri barani Afrika akiwa ametokea katika familia ya
Onsi Sawiris, yeye akiwa ni mtoto wa mwisho katika watoto watatu. Kaka
zake wawili ni Naguib na Samih.
Utajiri
wa Sawiris ni pauni bilioni 7.5 na inaonekana alianza kupambana na
biashara akiwa chini ya baba yake mzazi kuanzia mwaka 1982 kupitia
kampuni ya ujenzi ya Orascom Construction na mwaka 1995 akakabidhiwa
mikoba kuwa CEO na juhudi zake kubwa na ubunifu uliifanya kampuni hiyo
kukua kwa kasi kubwa.
Kadiri
siku zinavyosonga alizidi kujitanua kimasoko na kufikia kufungua baadhi
ya makampuni kadhaa Dubai ambayo yalizidi kumuongezea utajiri.
Sawiris
alizidi kujitanua katika biashara mbalimbali ukiachana na zile za
ujenzi lakini nyingine zilizojihusisha na michezo, mwaka 2015 kupitia
kampuni yake ya NNS Holding Sarl ya nchini Luxembourg alinunua baadhi ya
shea zilizoiwezesha kampuni hiyo kusimamia baadhi ya kazi za kampuni
kubwa ya michezo ya Adidas.
Julai
mwaka 2018, ikatangazwa kwamba Sawiris atakuwa ndiye Mwenyekiti wa
Klabu ya Aston Villa ya England akichukua nafasi ya aliyekuwa
mwenyekiti, Tony Pia.
Sawiris
alichukua nafasi ya uenyekiti baada ya kununua hisa za kiwango cha 55%
zikiwa chini ya Kampuni ya NSWE ambayo inaendeshwa na kampuni yake kubwa
ya NNS inayoshirikiana na bilionea mwingine wa Kimarekani Wes Edens.
Wakati
Forbes ilimtangaza mwaka jana kuwa tajiri namba nne barani Afrika, kuna
taarifa nyingine zimeeleza Sawiris amekuwa akikua haraka sana kiuchumi.
Kaka
yake mmoja, Naguib Sawiris pia ni mmoja wa matajiri, akanadiriwa kuwa
na utajiri wa dola milioni 2.9, na hii inawafanya kuwa familia tajiri
zaidi nchini Misri.
Kampuni
ya Orascom Telecom ya Sawiris imewekeza hadi nje ya Misri katika
masuala ya mawasiliano na zaidi ni katika nchi za Lebanon na Pakistan.
Sawiris
pia anamiliki kampuni kubwa ya mawasiliano ya Koryolink ambayo ni
kampuni ya mtandao wa simu kwa mfumo wa 3G nchini Korea Kaskazini.
Mwaka
2015, Sawiris alizidi kuwa gumzo zaidi duniani baada ya uamuzi wake wa
kununua kisiwa kilicho katikati ya Ugiriki na Italia kwa ajili ya
kujenga makazi ya wakimbizi ambao wengi wao wamekuwa wakivuka kutoka
Afrika kwenda Ulaya kupitia bahari ya Mediterranean na bahati mbaya
wengi wao wamekuwa wakifa maji.
Suala
la kuwa na watu karibu milioni 6 wanaomfuatilia katika akaunti yake ya
mtandao wa kijamii wa Twitter umemfanya pia kuwa mmoja wa watu maarufu
zaidi duniani.
Hii
inatoa nafasi kwa Watanzania kuona kuwa Samatta analazimika kuwa katika
presha kama mchezaji kwa kuwa anatambua ana deni kubwa.
Deni litaanzia kwa kocha akimtaka kuona anafanya vizuri, lakini kuna presha ya mashabiki ambalo hili ni jambo la kawaida.
Kwa
Samatta kwa kuwa ameshacheza Ulaya kwa zaidi ya misimu miwili, anaelewa
hata presha ya wamiliki kama Sawiris ambaye lazima atakuwa anataka
kupata mafanikio.
Hawezi kuwa anaingilia uchezaji wa timu au vinginevyo lakini mwisho wa msimu atataka kuona kikosi kimefanya vema zaidi.
Ndiyo
maana kocha kama Dean Smith anapoona kuna namna ya kujiokoa anaweza
kumshawishi mmiliki kama Sawiris kutoa fedha takribani pauni milioni 10
kumpata mchezaji kama Samatta akiamini atakuwa jibu la matatizo yake ya
ushambulizi.
Mabilioni
huwekeza katika mpira kwa sababu ya biashara lakini wako huwekeza
sababu ya mapenzi yao kwa mchezo huo ingawa kamwe hawakubali kupata
hasara kutokana na wanachokiwekeza. Huyu, ndiye bosi mpya bilionea wa
Samatta.










0 comments:
Post a Comment