“TUNA
stress, hatujalipwa mwaka mzima.” Hiyo ni kauli ya mmoja wa waamuzi
wanaochezesha mechi za Ligi Kuu bara msimu huu akifungukia sakata la
baadhi ya waamuzi kuonekana wakiboronga kwenye mechi za hivi karibuni.
Hivi
karibuni, kumekuwa na malalamiko makubwa kwa waamuzi hasa wanaochezesha
mechi za Ligi Kuu Bara kufanya maamuzi yasiyo sahihi huku kubwa likiwa
ni kwenye kutafsiri sheria ya kuotea.
Wakati
sakata hilo likiendelea, tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), juzi
lilitangaza kumfungia miaka mitatu mwamuzi namba mbili, Kasim Safisha
aliyezua utata katika mchezo wa ligi kuu kati ya Simba na Namungo kwa
kukubali bao lililofungwa na Meddie Kagere wa Simba ambalo lilionekana
mfungaji kabla ya kufunga alikuwa ameotea.
Akizungumza
na Championi Jumamosi kwa sharti la kutoandikwa jina lake, mmoja wa
waamuzi hao alisema: “Unajua nini, mara ya mwisho tumelipwa Januari,
mwaka jana, hadi leo Februari 2020, hatujalipwa tena.
“Yaani
hivi sasa tuna stress (msongo) za mishahara ndiyo maana unaona
kunatokea matatizo kama hayo kwa sababu tunachezesha mechi huku mawazo
yakiwa nje ya kile tunachokifanya, tunaziwaza familia zetu, mimi binafsi
nadai zaidi ya milioni moja, wapo ambao wanadai fedha nyingi zaidi
yangu.
“Kwa
bahati mbaya pia tumekuwa hatupewi majibu mazuri na viongozi pindi
tunapojaribu kudai maslahi yetu, waamuzi tumekuwa tukijigharamia wenyewe
nauli, malazi na chakula pindi inapotokea umepangwa kwenda kuchezesha
mechi nje ya mkoa wako.
“Watu
watusamehe tu, hatufanyi makusudi, inatokea tu bahati mbaya kama ilivyo
kwa binadamu wengine, kwa sababu mtu anakuwa anawaza atarudije nyumbani
huku akiwa hana fedha na wakati mwingine tunakopa ili tuweze kusafiri,”
alisema mwamuzi huyo.
Championi
Jumamosi lilimtafuta Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mnguto kuweka
sawa mzani juu ya madai hayo ya malipo ya waamuzi kwa muda mrefu ambapo
alikiri kweli wanadaiwa. “Kweli waamuzi wanatudai, hivi sasa tunafanya
mchakato wa kuwalipa stahiki zao zote, lakini hilo lisiwe sababu ya wao
kuchezesha vibaya,” alisema Mguto.

0 comments:
Post a Comment