Tuesday, October 26, 2021

 



IMEIBUKA sintofahamu ndani ya Simba kufuatia timu hiyo kutupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuchapwa mabao 3-1 na Jwaneng Galaxy ya Botswana jana Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Matokeo ya jumla yanakuwa 3-3 kufuatia Galaxy kufungwa 2-0 kwenye mchezo wa kwanza Jumapili iliyopita Jijini Gaborone, lakini Simba SC inatolewa kwa kuruhusu mabao zaidi nyumbani.
Mara baada ya mchezo huo jana, Mwekezaji wa klabu hiyo, Mohamed ‘ Mo’ Dewji’ alisema; “Kwa kuwa nimejiuzulu, sina nafasi ya kutoa uamuzi wowote Simba. Ninachoweza ni kutoa ni ushauri kwa mwenyekiti na bodi kuchukua hatua kali kwa wale ambao wanawajibika kwa upotevu wa mechi ya leo. Hii haikubaliki,”.


Kwa upande wake, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Crescentius Magori alisema; “Hii ni siku ya kiza totoro kwenye historia ya Simba! Usaliti ni kitu kibaya sana, hakivumiliki!,”.
Ni Mtendaji Mkuu wa klabu, Barbara Gonzalez pekee aliyekuwa ana mawazo chanya; “Leo tumejifunza somo la maana: ‘Kamwe usiwadharau wapinzani wako hadi filimbi ya mwisho itakapopulizwa.’ Hakuna dhamana katika mpira wa miguu. Bado ninaamini tuna timu nzuri. Kuteleza si kuanguka. Tutarudi tukiwa na nguvu zaidi!,”.
Wakati Galaxy inatinga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa, Simba itakwenda kumenyana na moja ya timu za Kombe la Shirikisho kuwania kucheza hatua ya makundi pia ya michuano hiyo midogo ya CAF.
Droo inatarajiwa kupangwa kesho Jijini Cairo  na Simba inatarajiwa kukutana na moja ya timu zilizovuka Raundi ya Pili Kombe la Shirikisho.
Hizo ni RS Berkane (Morocco), Enyimba (Nigeria), CS Sfaxien (Tunisia), JS Saoura (Algeria), Pyramids FC (Misri), Al Masry (Misri), Gor Mahia (Kenya), Marumo Gallants (Afrika Kusini), Coton Sport (Cameroon), Orlando Pirates (Afrika Kusini), Red Arrows (Zambia), DC Motema Pembe (DRC), Binga FC (Mali), Interclube (Angola) na ama Biashara United au Al Ahli Tripoli ya Libya.

0 comments:

Post a Comment