Elieth Edward ni mwanamke wa miaka 24, yeye ni mzaliwa wa Mwanza Kata ya kitangili Tanzania.
Tofauti na watoto wa kike, tabia na mienendo yake ilikuwa kama ya watoto wa kiume. Alivutiwa zaidi na michezo inayopendwa na wavulana.
"Nilipenda mchezo wa mpira wa miguu zaidi, nilipokua mdogo wakati wasichana wenzangu wanaigiza michezo ya kinyumbani, mimi nilikuwa nafuatilia soka. Nilikua na ndoto ya kuwa nyota wa mchezo huo siku za usoni "anakumbuka Elieth
Elieth ambaye alikulia eneo la Mwanza anasema kuwa alipata malezi mazuri, lakini pia kwa upande mmoja anasema kulikuwa na changamoto kwa sababu katika familia yao hakukuwa na mtu hata mmoja aliyekuwa akicheza wala kufuatilia mambo ya soka.
Kwa hivyo wazazi wake hasa mama yake hakuridhia uamuzi wake wa kujitosa kwenye ulimwengu wa soka.
Elieth alianza kuandamana na kaka yake kila mahali na wakati mwingi walijipata uwanjani wakishabikia timu mbalimbali za soka.
"Katika familia ya upande wa baba hakuna mtu hata mmoja aliyekuwa anacheza soka, ila katika familia ya mama yangu kuna watu wąchache waliojihusisha na mchezo huo wa mpira wa miguu, kwa hivyo sikutarajiwa kuzungumzia soka na nilipata wakati mgumu kwa kuwa nililazimika kujificha ili nifuatilie mchezo niliyoupenda "anasema Elieth.
Ila mwanadada huyu anasema kuwa mama yake mzazi hakuwa anapendelea mwenendo wake wa kuenzi soka.
Kwa sababu hiyo anasema kuwa alipigwa sana na mama yake kama njia ya kumkatisha tamaa ya kuacha soka.
"Siku nyingi mama alinichapa, kwani kuanzia darasa la tatu nilianza kucheza soka shule ya msingi, ila kila aliponichapa nilihisi msukumo usio wa kawaida kuendelea kufwatilia mchezo huo. Siamini leo hii mama ni shabiki wangu mkubwa kwenye kilabu ninayowakilisha "anasema Elieth
Tangu akiwa darasa la tatu aliendelea kucheza soka hadi alipoingia shule ya sekondari.Akiwa kidato cha pili alipata fursa ya kuwakilisha Tanzania kwenye timu ya taifa ya wachezaji wanawake walio chini ya umri wa miaka 18.
Vivyo hivyo aliwakilisha nchi hiyo kwa miaka mengine mitaut , akitumikia timu ya taifa hali kadhalika klabu ya Mash jijini Mwanza.
Kubeba Ujauzito
Mwaka wa 2019 akiwa na miaka 20 alipata ujauzito bila kupanga kwani yeye na mchumba wake hawakuwa tayari kwa uzazi. Lakini hakukata tamaa bali aliamua kubeba mimba hadi mwisho alipojifungua.
Haikuwa rahisi kwani tayari alikuwa anachezea timu ya taifa, kipindi hicho akiwa na mimba ni wakati timu ya taifa ya wanawake walio chini ya miaka 20 ilipata fusa ya kusafiri hadi nchini Nigeria kuwakilisha Tanzania katika mashindano ya soka ,yalikuwa ni mashindano ya kufuzu kwa Kombe la Dunia.
"Mimi nilisafiri kuelekea Nigeria nikiwa na ujauzito pia, nilipata nafasi ya kucheza kwa dakika tano wakati wa mashindano hayo, sikupata shida yoyote." anasema Elieth.
Mwanadada huyu anasema kuwa hata baada ya kurejea nchini aliendelea kusakata kabumbu katika ligi ya nyumbani na timu ya taifa hadi uja uzito wake ulipofikisha miezi sita .
Aliamua kuchukua mapumziko kwa ajili ya maandalizi ya kujifungua mtoto wake wa kwanza. Wakati huo anasema kuwa alihisi kana kwamba alikuwa na uzito wa mwili usio wa kawaida na pia alikuwa na magonjwa yanayowapata wanawake wakiwa na ujauzito. Ndipo akamua kuondoka kambini kwa muda.
"Mama alinishauri nipate mapumziko ili nisipate matatizo yoyote, baada ya mapumziko ya miezi kama miezi minne hivi nilijaaliwa mtoto wa kike,"anakumbuka Elieth.
Mtoto wake alipotimiza miezi mitatu, Elieth alianza kusomea mafunzo ya ukocha wa daraja la kwanza na la pili.
Mtoto alipofikisha miezi saba aliamua kumuachisha maziwa na kurudi kambini. Ni uamuzi ambao haukuwa rahisi kwake, ila hakuwa na budi kufanya hivyo kutokana na mapenzi ya soka.
Mwanadada huyu anakiri sio rahisi, lakini alikuwa na matumaini ya kufanikiwa katika mchezo wa soka, ndiposa akamua kumwachia mtoto mama yake mzazi na kurejea tena kambini.
"Kupata ujauzito sio kitu nilichopangia, lakini kwa upande mwengine niliona ni wakati mzuri wa kuwanyamazisha baadhi ya watu ambao walikuwa na mtazamo kuwa wanawake wanaspoti hawana uwezo wa kujifungua,''aliendelea kusema.
''Baada ya kusikia uvumi huo mitaani na maeneo mengine kwa muda mrefu, moyoni mwangu nilikuwa naomba nijaaliwe kuwa na mtoto ili wenye fikra kama hizo wakome kuzungumzia wachezaji wa soka hususan wanawake ."anasema Elieth.
Mwanadada huyu anasema baadhi ya watu waliokuwa wanamzunguka wakati huo walikuwa na maoni kwamba mwanamke anayecheza mpira wa miguu hana uwezo wa kuzaa.
Sababu kubwa Elieth anasema ni muonekano au umbo la wanawake wanaocheza soka.
Kutokana na mazoezi ya kila siku muonekano wao hubadilika na kuchukua umbo la wanaume. Ila anasisitiza lichs ys muonekano huokuwa wao ni kama tu wa wanawake wa kawaida.
''Niliamua kulea mimba yangu ili kuondoa dhana hizo kwani mwanamke ana uwezo wa kuzaa akiwa mzima. Haijalishi anafanya kazi gani. Kwa hivyo mimi na mzazi mwenzangu tulifikia uamuzi huo na hadi wa leo tunaendelea na majukumu ya kumlea mtoto wetu, licha ya kuwa bado hatujaanza maisha ya ndoa "anasema Elieth.
Unyanyapaa wa kuwa mwanamke mwanasoka
Elieth Edward anayewakilisha timu ya Fountain Gate iliyopo Dodoma katika kiwango cha ligi, wakati mwingi anajipata kambini.
Lakini anasema kuwa hali ya wanawake kujitosa kwenye ulingo wa soka, unawafanya baadhi ya watu katika jamii kuwa na maoni tofauti juu ya muonekano wao.
Aidha mwanadada huyu anasema kuwa mchezo wenyewe unabadilisha umbo la mwanamke na watu wengi wamekuwa wakitumia maneno ya kudhalilisha dhidi ya wanawake kama yeye.
"Kwa mfano utasikia wengine wanatuita dume jike kutokana na muonekano wa miili yetu. Mazoezi ya mara kwa mara ndio yanabadilisha muonekano wetu. Lakini mimi ni mwanamke kama mwanamke mwengine sina tofauti yeyote "anasema Elieth
Mwanamichezo huyu anasema kuwa kuna dhana ya za kuwa mtoto wa kike anapocheza soka anaweza kushindwa kutekeleza majukumu ya kina mama nyumbani ila yeye anapinga madai hayo.
"Ndio kuna vile miili yetu inakaa tofauti , lakini hiyo haimaanishi kuwa tumebadili maumbile yetu. Pia dhana kwamba tunajaribu kuwa wanaume sio sahihi na ni kitu ambacho ningependa kusema hadharani, sisi tunapenda kucheza soka kwa mapenzi yetu na hili haliwezi kuwa kikwazo cha sisi kuwa mama wa familia "Elieth anasema
Elieth anasema kuwa ni muhimu wanawake duniani wajiamini, licha ya changamoto wanazopitia. Anasisitiza kuwa kuwa ni jambo zuri kuitwa mama, lakini isiwe kikwazo cha wao kufikia ndoto zao maishani.
0 comments:
Post a Comment