HAIKUWA kazi rahisi kuwashawishi Watanzania kuangalia mechi za Ligi Kuu na kuacha Ligi ya England, au kulazimika kuangalia kwa pamoja.
Ni kazi ngumu iliyofanyika kuwashawishi na kwa sasa Ligi ya Tanzania ni moja kati ya ligi zinazoangaliwa na watu wengi si hapa tu, bali ukanda wote huu wa Afrika Mashariki na Kati hadi Kusini.
Ni watu waliamua kuacha kazi na kufanya kazi, kuna watu waliwashawishi mashabiki kwa kuwekeza kwenye soka, yapo makampuni mengi yameanza kujitokeza kudhamini klabu pamoja na soka lenyewe kwa ujumla kupitia Shirikisho la Soka nchini (TFF).
Wapo watu binafsi ambao nao baada ya kuona soka limeanza kuwa na mvuto kwa mashabiki, wamewekeza kwenye klabu walitoa pesa nyingi, si kwa ajili ya wao kupata faida, bali kuufanya mchezo wa soka kuendelea kuwa kituvio, lakini kuendelea kutengeneza vijana kwa ajili ya timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Wakati TFF, makampuni, na wadau wakilifanya soka la Tanzania kung'ara ndani na nje ya mipaka ya nchi, kumeanza kutokea mambo ya ajabu yanayotaka kurudisha soka la Tanzania kwenye zama za giza. Si wengine ni baadhi ya waamuzi.
Waamuzi ni moja kati ya watu ambao wanafanya soka la nchi liendelee, kuwa na ligi bora au mbovu, pia kutoa mwakilishi bora kwenye mechi za kimataifa, kutoa mwakilishi dhaifu na feki.
Pamoja na kwamba Ligi Kuu ya Tanzania imeanza kwa mvuto, kuwa ngumu kutokana na kila timu kuonekana kujipanga kisawasawa, huku zikichagizwa na pesa zilizowekwa na wadhamini Azam Media, pamoja na NBC, baadhi ya waamuzi wameonekana kuanza kuharibu mapema kabisa.
Hata mzunguko wa kwanza haujafika kumekuwa na matukio mengi ambayo waamuzi wametoa maamuzi yasiyo sahihi na kuzipokonya timu ushindi au sare.
Tuliona mechi ya Yanga dhidi ya Azam, Idd Nado akikwatuliwa ndani eneo la hatari, lakini mwamuzi kwa sababu zake alishindwa kutoa penalti. Fiston Mayele alizawadiwa penalti baada ya yeye mwenyewe kushika mpira.
Mbaraka Yusuph alifunga bao la kuotea dhahiri, akiisawazishia Kagera Sugar, ingawa kwa bahati Geita Gold ikapata bao la pili baadaye na timu yake kulala kwa mabao 2-1.
Kali kuliko yote, mwamuzi Abel William kutoa mkwaju wa penalti kwa Yanga, baada ya Feisal Salum kunyang'anywa mpira kirahisi ndani ya 18.
Ukilirudia tukio lile hata mara 100, hakuna hata dalili za kusema ilipashwa kuwa penalti. Mchezaji aligusa mpira na Fei Toto alianguka mwenyewe.
Ukishangaa ya Mussa utaona ya Firauni, sasa hata hiyo penalti yenyewe ilivyopigwa hata mechi za mchangani haiwi vile. Ni aibu kubwa kwa soka la Tanzania ambalo linatazamwa hata nje ya mipaka yetu.
Wakati Saido Ntibazonkiza anapiga penati hiyo, jumla ya wachezaji watano wa timu zote mbili walikuwa wameingia ndani ya dimba. Fei Toto alionekana kuingia kiasi cha kutaka kumpita mpigaji na bado likaruhusiwa kuwa ni bao, badala ya kurudiwa.
Ni tukio lililoleta vurugu hata kwenye vibanda umiza. Kuna baadhi ya mashabiki kwenye kibanda umiza walianza kuondoka, wengine waliongea maneno makali, ilibaki kidogo hata mwenye kibanda apigwe. Wengine wakitamka kabisa kuwa bora kuangalia mpira wa Ulaya ambao hauna makandokando, lakini si huu wa Tanzania.
Unaanza kujiuliza kama hawa watu wangekuwa uwanjani sijui ingekuwaje?
Ni kweli kuna baadhi ya matukio hata waamuzi wa nje wanasaidiwa wa VAR, lakini kuna mengine waamuzi wanakuwa hapo hapo, ila wanababaika kutoa maamuzi yasiyo sahihi.
Unajiuliza kama sheria za soka huwa zinabadilika kutokana na timu inayocheza au zinafanya kazi kwa wote.
Inafikirisha mwamuzi aliyekataa kutoa penalti kwenye mechi ya Simba dhidi ya Ruvu Shooting baada ya Bernard Morrison kukatwa ndani ya eneo la hatari, na yule aliyetoa penalti kwa beki kumnyang'anya Fei Toto mpira.
Makocha, wachezaji, wadhamini na wafadhili wanafanya kazi kubwa ili kuufanya mpira kuwa na thamani, lakini unaonekana kuharibiwa na baadhi ya waamuzi kwa sababu wanaozijua wao wenyewe.
Ifike wakati sasa TFF, Bodi ya Ligi (TPLB) na Chama cha Waamuzi (FRAT) kilinde thamani ya ligi yetu kwa kuwapa adhabu kali waamuzi wenye tabia hii ili iwe fundisho kwa wengine. Isipochukua hatua kesho na keshokutwa tunaweza kushuhudia vituko vingine zaidi ya hivi tunavyoanza kuvishuhudia ligi ikiwa ndiyo kwanza bado asubuhi.
Na mashabiki hawatoiamini tena na kuanza kukimbia ndiyo watu waanze kutafuta nini chanzo cha kupungua mashabiki viwanjani na kwenye kibanda umiza wakati 'mchawi' anajulikana.
Waamuzi waache kutengeneza matokeo, kwa sababu hapa anatafutwa mwalikishi wa nchi. Apatikane kwa uwezo wake ili akaiwakilishe nchi vizuri na si wa kuchongwa, matokeo yake mechi za kwanza tu tunatolewa, huku kila mtu na wachambuzi wakitoa sababu nyingi ambazo hazipo.
Kumbe nchi ilikuwa na mwakilishi feki, na huko hakuna kubebana. TFF ichukue hatua kali kwa waamuzi hawa kwa ajili ya kulilinda thamani ya soka la Tanzania.
0 comments:
Post a Comment