
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania, imekutana Jumapili Julai 30, 2017 katika
Ukumbi wa Hosteli za TFF, zilizopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala
jijini Dar es Salaam yaliko Makao Makuu ya shirikisho.
Kikao hicho, kimepitisha mambo
mbalimbali ambako miongoni mwake ni mabadiliko ya Kanuni za Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara. Miongoni mwa kanuni ziliguswa ni ya kuhusiana na
kujali afya za wachezaji pamoja na mikataba wanayoingia na klabu.
Hivyo, TFF imeagiza msimu wa
2017/18 mchezaji atayesajiliwa hatapewa leseni ya kumruhusu kucheza
mashindano husika kama vile Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania (VPL), Ligi
Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili kama hatakamilisha masharti
makuu matatu kwa mujibu wa kanuni.
Masharti hayo ni kukatiwa Bima ya
Matibabu, Kuidhinishwa afya yake ambayo mara baada ya fomu yake
kupitishwa na Kamati ya Tiba ya TFF kwa mujibu wa Kanuni ya 18 (1) ya
Ligi Kuu na Mkataba wake wa maandishi ‘hardcopy’ kuwasilisha TFF kwa
mujibu wa Kanuni ya 69 (8) ya Ligi Kuu.
Kama kuna timu haitakidhi japo
sharti moja kati ya hayo, basi mchezaji wake hatapewa leseni ya kucheza
kwa msimu husika. Kaimu Rais wa TFF, Wallace Karia, akifunga hoja hiyo,
alisisitiza akisema: “Wakati huu hatutaki siasa. Tusimamie kanuni hizi,
hatutaki kuleta mchezo msimu huu.”
Hayo yamekuja baada ya klabu
kutakiwa kuwawekea Bima ya Matibabu kwa mujibu wa kanuni ya 18 (1)
inayosema: “Kila Klabu ina wajibu wa kuwawekea wachezaji wake bima ya
matibabu na fidia kutokana na ajali michezoni. Klabu itakayokiuka kanuni
hii itakuwa imepoteza sifa ya kuwa klabu ya Ligi Kuu, na usajili wa
wachezaji wa timu yake hautathibitishwa na haitashirikishwa katika Ligi
Kuu.
Kuhusu Mikataba kwa mujibu wa
Kanuni ya 69 (8), Kamati ya Utendaji imekubaliana kwamba: “Mikataba yote
ya wachezaji ambao haujasajiliwa na kuthibitishwa na TFF,
hautatambuliwa.”
Kadhalika, kuhusu wachezaji wa
Kigeni kwa mujibu wa Kanuni ya 57 (5), kitasomeka kama ifuatavyo:
“Mchezaji ye yote wa kigeni anayesajiliwa katika Ligi Kuu atalipiwa ada
maalumu ya Sh milioni mbili (Sh 2,000,000) kwa msimu kwa mchezaji mmoja
ili usajili wake uweze kuthibitishwa na kuruhusiwa kucheza.
Gharama za awali zilikuwa ni dola 2,000 za Marekani (sawa na Sh. 4.5 milioni.) kwa mchezaji mmoja.
Kadhalika, sasa kwa mujibu wa
kanuni ya 13 (6) Klabu Mwenyeji itakuwa na nafasi ya kuweka mpaka
mabango 10 ya Mdhamini/Wadhamini wake. Ukubwa wa bango moja lile lenye
vipimo vya 6m x 1m.
Kama timu ni mgeni katika mchezo
husika, ana uwezo kufanya makubaliano na mwenyeji wake akampa nafasi
katika hayo 10 ambayo yameruhusiwa kikanuni.
Aidha, Kanuni ya 14 imeongezwa
kipengele kimoja. Kanuni ya 14 (48) Klabu ina wajibu wa kushirikiana na
mdhamini wa matangazo ya televisheni ikiwemo kupata picha za wachezaji
na benchi la ufundi kwa ajili ya maandalizi ya mechi zao.
Na Kanuni 14 (49), inasema:
TFF/TPLB itachukua hatua kwa ukiukwaji wo wote wa taratibu za mchezo
kama zilivyoanishwa kwenye Kanuni ya 14 kwa kutoa onyo kali au karipio
au kutoza faini kuanzia Sh. 200,000 (lakini mbili) mpaka Sh. 300,000
(laki tatu), na/au kufungia mchezo isiyozidi mitatu (3) au kipindi
kisichozidi miezi mitatu (3) kwa mchezaji, kiongozi au timu.
Katika hatua nyingine, Kamati ya
Utendaji imeridhishwa na maandalizi ya Mkutano Mkuu ujao wa TFF ambako
pamoja na mambo mengine utakuwa na ajenda ya Uchaguzi Mkuu wa shirikisho
unaotarajiwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu.
Mjumbe wa FIFA, Solomon Mudege
alikuwa nchini kwa siku ya Jumamosi ambako alipata fursa ya kuzungumza
na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison
Mwakyembe; Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Yussuph Singo pamoja na
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji wa TFF wakiongozwa na Kaimu Rais Wallace
Karia.
Mara baada ya kupata maelezo ya
kuridhisha kutoka kwa wanafamilia hao wa mpira wa miguu ambao baadhi yao
alikutaa nao mmoja baada ya mwingine, alibariki mchakato wa uchaguzi
uendelee na Kamati ya Utendaji imetangaza kuwa utafanyika Ukumbi wa St.
Gasper mjini Dodoma.
Mudege alikuwa nchini kuangalia
hali maendeleo ya mpira wa miguu nchini hasa katika utawala, lakini kwa
kuwa uongozi uliokaimu madaraka umefuata taratibu, kanuni na sheria
tangu mwanzo, mjumbe huyo aliridhia mchakato wa uchaguzi na shughuli
nyingine ziendelee kama zilivyopangwa.
0 comments:
Post a Comment