BILIONEA kijana Afrika na mmiliki wa mojawapo ya klabu maarufu ya soka Afrika mashariki Simba SC – Mohammed Dewji amezungumza
kwa mara ya kwanza kuhusu sakata lake la kutekwa nyara mwaka jana na
namna alivyotishiwa maisha yake nchini Tanzania.
Katika mahojiano maalum na ya kipekee na BBC Swahili, Mo ameeleza
kuwa kwa kipindi kizima, alihisi kwamba kuna uwezekano mkubwa hatoweza
kutoka salama na kuwa mwisho wake wa maisha unakaribia.
“Saa 24 za kwanza baada ya kutekwa zilikuwa kama mwezi. Imani ndio kitu kikubwa kilichonisaidia katika kipindi kizima.”
Katika kuikumbuka siku hiyo, Mo ameeleza: “Walinifunga macho, miguu na mikono kwa siku tisa. Tulikuwa hatuongei sana, walikuwa sio watu wa hapa.
“Walikuwa wakinitisha na kuniweka bastola kwenye kichwa na kuniambia wataniua.” ameeleza mfanyabiashara huyo.
Mwaka jana mwezi Oktoba, Dewji alitekwa na watu wasiojulikana mjini Dar es Salaam. “Kufunga mlango
(wa gari) tu, kugeuka nimekuta watu wanne ambao wamevaa mask nyeupe –
wamefunika uso, wakapiga bunduki juu mara mbili halafu wameniwekea
bunduki.”
Anasema
awali alidhani ni jaribio la kutaka kuibiwa gari, na hakuwa na budi
kufuata maagizo alipoambiwa alale chini kwenye sakafu. “Kwenye sekunde
sitini hivi, hao watu wamekuja wamenibeba na kuniweka ndani ya gari.”
Anasema
kilichofuata katika safari hiyo anayosema iliyokuwa ngumu, watekaji
wake walimvua nguo kwa kuhofia huenda ana kifaa cha kutambua anakokwenda
yaani tracker na kumfunga mikono na miguu na kwenye dakika 20
wakamfikisha katika nyumba.
“Niligundua kuwa lugha wanayotumia sio lugha ya Tanzania,
ilikuwa ni geni. Asubuhi walikuwa wananifungua mikono wananifunga
mbele, lakini usiku ndio kulikuwa na mitihani walikuwa wananifunga
nyuma. Na wakikufunga nyuma maanake huwezi kulala, lazima ulale kulia au
kushoto.”
Mo
anasema alikuwa akitoa ushirikiano kwa kila alichotakiwa kufanya.
Kikubwa anasema alikuwa akimuomba Mungu atoke salama. Siku ya tisa
anasema “walinisukuma pale Gymkhana na nikasikia gari limeondoka.”
Kwa muda wote alipewa tu kipande cha khanga aliyotumia kujifinika mpaka siku walipomuachilia ndiyo aliyotumia pia kujifunika.
Mo Dewji alitekwa
Oktoba 11 2018 na watu wasiojulikana alfajiri wakati alipokuwa
akielekea mazoezini alipofika katika hoteli moja ya kifahari katika eneo
la Oysterbay jijini Dar es Salaam kama ilivyo ada yake kila siku
alfajiri kwa ajili ya kufanya mazoezi ya viungo.
Siku
tisa baadaye, Dewji alirejea nyumbani salama. Kamanda wa Polisi wa
Kanda ya Dar es salaam Lazaro Mombasasa aliyemtembelea Dewji
kuthibitisha kurejea kwake nyumbani, alisema watu waliomkamata walikuwa
na lafudhi ya mojawapo ya lugha za mataifa ya Kusini mwa Afrika.
Maswali
ambayo hadi leo yamesalia kufuatia mkasa wa kutekwa kwake MO ni:
Kwanini ametekwa? Nani aliyemteka? Kwanini hakuwa na mlinzi? Washukiwa
kadhaa wamekamatwa, na baadhi yao kuachiwa baada ya kuridhishwa na
upelelezi wa maafisa wa usalama.
Aliyekamatwa
hivi karibuni ni dereva wa teksi Mousa Twaleb aliyefikishwa mahakamani
nchini akihusishwa na utekaji wa mfanyabiashara huyo maarufu.
Mkuu
wa polisi wa Dar es Salaam, kamanda Lazaro Mambosasa alieleza kwamba
bwana huyo ambaye pia ni dalali wa nyumba ndiye ‘aliyewakaribisha mjini
watekaji wa Mo na kuwapangisha nyumba ambayo alidai kuwa waliitumia
kumficha Mo baada ya kumteka’.
Kuhusu
uchunguzi ulipofikia, Mo amesema kwamba hafuatilii sana uchunguzi ambao
unafanyika nchini kufuatia mkasa huo ulitokea mwaka jana mwezi kama huu
Oktoba.
Ameeleza
kwamba amekuwa tu akisoma kwenye vyombo vya habari na anachokifahamu
kufikia sasa ni kwamba kuna mtu mmoja au wawili kutoka Msumbiji, mmoja
wa Afrika kusini na mwingine Mtanzania ambaye amewekwa ndani. “Mimi ni
mtu nasamehe watu, siweki vitu ndani ya moyo wangu”.
MO DEWJI NI NANI?
Mo alizaliwa tarehe 8 Mei mwaka 1975, ikiwa na maana kwamba kwa sasa ana miaka 43.
Alizaliwa eneo la Ipembe, Singida maeneo ya katikati mwa Tanzania.
Kwa mujibu wa jarida maarufu la masuala ya fedha la Forbes, ana utajiri wa dola bilioni 1.5.
Ni wa pili miongoni mwa watoto sita wa Gulamabbas Dewji na Zubeda Dewji.
Alisomea
elimu ya msingi katika shule ya msingi ya Arusha na baadaye akasomea
elimu ya sekondari katika Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) jijini
Dar es Salaam.
Alisomea masomo zaidi ya sekondari Marekani katika jimbo la Florida mwaka 1992.
Alisomea
chuo kikuu cha Georgetown jijini Washington DC na kuhitimu mwaka 1998
akiwa na shahada ya kwanza katika biashara ya kimataifa na fedha, na
masuala pia ya dini.
Baada
ya kufuzu, alirejea Tanzania na kuanza kushiriki katika usimamizi wa
kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL) iliyoanzishwa na
babake miaka ya 1970.
Alihudumu kwa miaka miwili kabla ya kuwa afisa mkuu mtendaji wa kampuni hiyo, wadhifa ambao ameendelea kuushikilia hadi sasa.
Dewji
pia ni mpenzi wa michezo na amewekeza katika klabu ya mpira ya Simba
Sports Club inayocheza katika Ligi Kuu ya Tanzania ambapo ni mfadhili
mkuu kwa sasa.
Mo ndiye tajiri namba moja Afrika Mashariki, na pia miongoni mwa matajiri wenye umri mdogo zaidi Afrika.
Tathimini ya ukuwaji wa uchumi na Biashara Tanzania
Katika kutathmini kuhusu ukuwaji wa uchumi Tanzania Mo ameeleza kuwa kutokana mtazamo na dira ya nchi, hali ni ya kutia moyo.
“Tanzania
inakuwa kwa 6.5% dhidi ya wastani wa ukuwaji wa uchumi Afrika, ambao ni
3%. Mfumuko wa bei uko chini ya asilimia 3.5%, hii ni habari nzuri.”
Kwa
mujibu wa benki ya Dunia, Tanzania imeendeleza ukuwaji wa uchumi katika
muongo mmoja uliopita, kwa wastani wa kati ya 6% – 7% kwa mwaka.
Kadhalika,
idara ya takwimu nchini Tanzania inaeleza kuwa pato jumla la nchi
lilikuwa ni 7% mwaka jana, ongezeko kutoka 6.8% mnamo 2017.
Hata hivyo, mfanyabiashara hiyo ameeleza kwamba changamoto hazikosekani.
Mojawapo kubwa amelitaja ni ajira, na pia uwekezaji mdogo katika seta kama kilimo na viwanda.
Swali kubwa anauliza Mo ni: “Kwanini viwanda vimefungwa, kwanini havizalishi?
Jibu lake anasema, ili kufanikiwa matatu haya ndio yanahitajika:
Tatizo
kubwa anasema linalopaswa kuulizwa ni ‘kwanini mali ghafi husafirishwa
nje mfano, 90% ya pamba nchini inayowagusa asilimia kubwa ya wakulima na
tunazalisha 10%’.
Mfumo anasema ni mzuri lakini tatizo anafafanua ni udanganyifu na ushindani wa haramu katika biashara.
Anapendekeza
serikali iweke sera zitakazosaidia wafanyabisahara katika sekta hiyo
kuwawezesha kuzidisha uzalishaji wa biashara na kusaidia kudhibiti mali
za nchi.
Siri ya ufanisi wa Dewji?
Kujituma: Anaeleza
ni lazima vijana wawe na nidhamu ya kuwa na muda wa kulala, kuamka na
kufanya kazi. Binafsi anaeleza kuwa huamka kila siku saa kumi na moja
alfajiri na hufanya kazi kwa saa 80 kwa wiki.
Kusoma
zaidi: Anausia watanzania hususan vijana wajenge mapenzi ya kusoma.
“Watanzania hatupendi sana kusoma, ni heri kusoma umbea kuliko (content)
itayotuongezea elimu.”
Kujikita
katika biashara ndogo: Hii ni kwa mudhumuni ya kutengeza akiba ambayo
anaeleza inakuwa ni msingi kwa vijana wanapokwenda kutafuta mikopo
kujiendeleza. Inakuwa na uzito zaidi katika kufanikiwa kupata mitaji ya
kupanua biashara zaidi.





0 comments:
Post a Comment