LICHA
ya kutoka kwenye majeraha ya goti, kocha na mchezaji wa zamani wa
Simba, Abdallah Kibadeni amesema anaona wazi kuwa mshambuliaji wa timu
hiyo, John Bocco anapiga hat trick safi dhidi ya Yanga leo.
Kama
Bocco atafunga hat trick leo pale Uwanja wa Taifa, basi ataifikia
rekodi ya Kibadeni ya kufunga hat trick dhidi ya Yanga ambayo aliiweka
Julai 19, 1977.
Kibadeni
alifunga hat trick hiyo na kuisaidia Simba kushinda mabao 6-0, alitupia
mabao yake dakika za 10, 42 na 89. Mabao mengine ya Simba yalifungwa na
Jumanne Hassan ‘Masimenti’ dakika za 60 na 73 na lingine lilikuwa la
kujifunga la Selewa Sanga wa Yanga dakika ya 20.
Kibadeni
alisema kuwa, anaona wazi Bocco ana nafasi kubwa ya kufunga mabao
matatu licha ya kuwa ametokea kwenye majeraha yaliyomfanya akae nje kwa
muda mrefu.
“Nampa
nafasi kubwa Bocco kuweza kufunga mabao matatu katika mchezo huo kwani
kiwango chake kipo vizuri licha ya kutoka majeruhi, hivyo akijitahidi
atafunga mabao matatu,” alisema Kibadeni na kuongeza:
“Simba
ipo vizuri sana kwa sasa tofauti na Yanga ambayo kikosi chake sio
kipana kama Simba, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kuweza kuibuka
washindi zaidi ya bao moja katika mchezo wa kesho (leo).
0 comments:
Post a Comment