by alanus
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemuagiza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison
Mwakyembe alifanyie mapitio Baraza la Michezo Tanzania (BMT) na iwapo
hatoridhika na utendaji wake alivunje.
“Ninamuagiza Waziri mwenye dhamana
kufanya mapitio na kutathmnini upya utendaji kazi wa Baraza la Michezo
Tanzania juu ya usimamizi wake wa michezo nchini na kama hataridhika,
anayo mamlaka ya kulivunja Baraza hilo.”
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo
(Jumatano, Julai 5, 2017) katika hotuba yake ya kuahirisha Mkutano wa
Saba wa Bunge mjini Dodoma.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano
haitafumbia macho usimamizi mbovu na utawala wa michezo usiojali maslahi
ya Taifa. “Serikali imeazimia kuimarisha utendaji kwa vyombo vya
michezo nchini ili kila mwenye dhamana awajibike ipasavyo.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
ameipongeza timu ya vijana walio chini ya umri wa miaka 17, Serengeti
Boys iliyoshiriki na kutoa upinzani mkubwa kwenye mashindano ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika.
Amesema licha ya timu hiyo
kumaliza ikiwa na jumla ya pointi 4 sawa na timu iliyoshika nafasi ya
pili, ila Vijana hao wameonesha vipaji na uzalendo wa hali ya juu kwa
nchi yao.
“Msisitizo wangu kwa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni kuendelea kuwatunza vijana hao, na
kusimamia vilabu vya michezo nchini kuwekeza kwenye soka la vijana ili
tujenge timu imara kwa miaka michache ijayo.”
Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua umuhimu wa michezo kwa afya, umoja wa kitaifa na kama fursa ya ajira kwa vijana nchini.
“Wiki iliyopita, mkoani Mwanza
yamehitimishwa mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA. Wananchi wa Mwanza
na Watanzania kwa ujumla wamejionea uwezo wa kimichezo, vipaji na
hamasa kubwa iliyopo miongoni mwa vijana wetu kutumia vipaji vyao. “
Amesema Serikali itaendelea
kuratibu michezo shuleni, ikiwa ni pamoja na kusimamia ufundishaji wa
michezo kama somo. “Maelekezo yetu ni kwamba kila Mkoa uwe na shule
angalau mbili zenye mchepuo wa michezo na walimu wenye sifa stahiki za
kufundisha michezo.”
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewaagiza
Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini, wahakikishe kwamba kila shule
inakuwa na viwanja vya michezo mbalimbali ili kuwapa fursa wanafunzi
kushiriki michezo ili kupandisha na kuinua vipaji vyao.
Pia Waziri Mkuu alitumia fursa
hiyo kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli kwa kuunga mkono
jitihada za michezo nchini kwa dhamira yake ya kujenga uwanja mkubwa wa
michezo mjini Dodoma kwa kushawishi mataifa rafiki kama vile Morocco
ambao wanajenga uwanja huo.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
- L. P. 980,
40480 – DODOMA.
JUMATANO, JULAI 05, 2017
0 comments:
Post a Comment