Friday, September 8, 2017

Na Thomas Ng’itu
KLABU ya African Lyon inayomilikiwa na Mkurugenzi machachari Rahim Kangezi ‘Zamunda’, imeshuka daraja lakini ni bado ipo katika ligi kuu baada ya wachezaji wake wote nyota waliokuwa katika kikosi hicho kuendelea kubaki katika ligi kuu.
Shaif Dauda Website baada ya kufanya uchunguzi wake imegundua kuwa Lyon baada ya kushuka daraja, imebakisha nyota wake wengi  kwenye ligi hivyo ni kama bado inaendelea kuwepo kama ambavyo inaonekana katika orodha hii ya chini.
Youthe Rostand
Kipa huyu raia wa Cameroon alianza kuzitoa udenda muda mrefu vilabu vyenye pesa katika ligi kuu Bara, lakini kulikuwa na vuta ni kuvute kati yake na Mkurugenzi wa Lyon Rahim Kangezi kabla ya kumwaga wino Jangwani.
Rostand hivi sasa yupo Yanga na anatarajiwa kuwa na msaada katika timu hiyo kutokana na yeye pekee kuwa na uzoefu mkubwa zaidi ya Beno Kakolanya na Ramadhan Kabwili, hivyo aningia moja kwa moja katika orodha ya wachezaji wa Lyon wanaoendelea kuwepo katika ligi kuu.
Miraj Adam
Beki huyu mwenye uwezo wa kucheza nafasi ya beki wa kulia na  kati, naye anaingia katika orodha ya wachezaji wa Lyon waliobaki katika ligi kuu baada ya kusaini katika klabu ya Singida United iliyopanda daraja.
Miraj alikuwa mchezaji tegemeo katika upande wa kulia katika kikosi cha Lyon na katika mechi za ligi kuu alikosa mechi mbili tu za mwanzo, hivyo usajili wake katika kikosi cha Singida kutawasaidia kutokana na uzoefu wake baada ya kucheza Simba, Coastal Union na Lyon pia.
Peter Mwalyanzi
Kiungo huyu alianza kuonekana akiwa katika uzi wa Mbeya City, aling’ara mpaka kufikia hatua ya kusajiliwa na kalbu ya Simba, akiwa Simba hakupata nafasi kubwa sana ya kuonyesha kiwango chake na akatua Lyon msimu uliopita.
Akiwa na Lyon mwanzoni hakupata nafasi ya kucheza mara kwa mara kutokana na aina ya wachezaji waliokuwa katika kikosi hicho, lakini katika mechi ambazo amecheza alionyesha uwezo kiasi cha Kagera kuvutiwa na huduma yake na kumsajili.
Mwalyanzi anatakiwa aonyeshe kwa mashabiki wa Simba waliokuwa wanambeza kuwa amechuja, yeye ni bora akiwa na Kagera na hio inawezekana kutokana na jinsi ambavyo kambi ya Kagera ‘Sobibo’ inavyomlazimisha mchezaji kufanya mazoezi na kupumzika.
Omary Abdallah ‘Daga Shenko’
Straika huyu alifunga bao pekee katika mchezo wa Lyon dhidi ya Simba walipolala kwa mabao mawili kwa moja katika uwanja wa Taifa, alikuwa ni mchezaji anayesumbua akiwa na jezi yake namba nane mgongoni.
Alianza katika klabu hiyo tangu akiwa mdogo akitokea katika kikosi cha vijana cha timu hiyo, lakini ameondoka akiwa mchezaji huru bila timu hiyo kupokea pesa yoyote kutoka kwa Kagera, Kagera watafaidi matunda ya mchezaji huyu kutokana na kwamba bado ana umri mdogo alafu ana uchu wa maendeleo, kwa namna moja ama nyingine kambi ya Kagera itamkomaza zaidi.
Awadh Salum ‘Awadh Mido’
Awali aliichezea timu ya vijana ya Yanga iliyokuwa inanolewa na kocha Salvatory Edward kwa kipindi hicho, baada ya kuona kuwa ni ngumu kupata namba kutokana na kuwa na viungo kama Haroun Niyonzima aliamua kutimkia katika kikosi cha Lyon.
Akiwa Lyon alionyesha uwezo wake katika mechi zake alizocheza kwa kuweza kupigana vikumbo na viungo bora wa Simba,Yanga na Azam, alitakiwa na Kagera lakini alichungulia nafasi yake ya kucheza na baadaye akaamua kumwaga wino katika klabu ya Njombe Mji kwaajili ya msimu.
Hamad Manzi ‘Yahya Toure’
Kiungo mwenye umbo kubwa aliyekuwa anasumbua katika dimba la kati katika nafasi ya kiungo mkabaji, alikuwa naweafanya viungo wa Lyon wacheze kwa uhuru,amemwaga wino katika klabu ya Lipuli ambayo inaonekana kufanya usajili wa fujo baada ya kukaa kimya.
Manzi atawasaidia Lipuli kutokana na aina ya uchezaji wake, huku akiwa tayari ameshaanza kukomaa kwa kucheza mechi za ligi kuu na kombe la Fa tena kwa kukutana na viungo bora katika ligi kuu bara.
Venance Ludovick
Kabla hakujaibuka utata juu ya leseni yake ya kufanyia kazi kati ya Mbao na Lyon, mchezaji huyu alionyesha kiwango cha juu katika mechi zake alizocheza akiwa Mbao na hata Lyon, ni mchezaji ambaye ana spidi na uwezo wa kumiliki mpira kuufanya ambavyo anataka.
Hakucheza msimu uliopita katika mechi za Lyon licha ya kuwa baadaye alifunguliwa kuendelea kucheza, katika msimu ujao atakuwa katika kikosi cha Kagera, kwa aina yake ya uchezaji anaweza kufanya makubwa akiwa ndani ya kikosi hicho.
Mussa Nampaka ‘Chibwabwa’
Kiungo huyu alishawahi kuichezea Mtibwa Sugar akiwa katika kiwango kizuri sana hadi kukaibuka tetesi kuwa anatakiwa kujiunga na kikosi cha Yanga, lakini aliendelea kubaki katika kikosi cha Mtibwa.
Msimu uliopita alisaini Lyon lakini hakupata nafasi ya kuwepo katika kikosi hicho licha ya kuwa alikuwa amesajiliwa, mara chache alikuwa akionekana katika mazoezi ya timu hiyo lakini sio katika mechi, msimu ujao atakuwa ndani ya uzi wa Lipuli, aataisaidia klabu hiyo kwa muunganiko wake na Hamad Manzi ambaye alikuwa nae katika kikosi cha Lyon.
Hassan Isihaka
Aliwahi kuwa nahodha wa kikosi cha Simba, alikuwa katika kiwango cha juu akiwa kwenye kikosi hiko, lakini alijikuta anaondoka katika kikosi hicho na kutua Lyon akiwa kama mchezaji aliyetolewa kwa mkopo.
Akiwa Lyon alifanya vizuri na kuonyesha kuwa ni kati ya mabeki wazuri wa kati katika ligi kuu,msimu ujao atakuwa katika kikosi cha Mtibwa Sugar kikosi ambacho kinanolewa na Zubery Katwira mtu ambaye alipendekeza beki huyu kusajiliwa hivyo atazidi kuwa bora na kuonyesha makali yake.
Abdalah Mguhi ‘Messi’
Naye ni miongoni mwa nyota waliowahi kukipiga katika timu ya vijana ya Yanga, alipandishwa katika kikosi cha wakubwa na kupewa jina la ‘Messi’ lakini baadaye alitolewa kwa mkopo Lyon kipindi ikiwa daraja la kwanza.
Alicheza Lyon ikiwa daraja la kwanza na baadaye akafanikiwa kupanda na timu hiyo katika ligi kuu msimu uliopita, alikuwa ni kati ya wachezaji ambao wanapeleka mashambulizi na kuisaidia lyon kufanya mashambulizi ya kushtukiza, lakini msimu ujao ataonekana akiwa katika uzi wa Kagera Sugar.
Rehan Kibingu
Yeye hakuwa na hiyana baada ya kuona dili la kujiunga na Lipuli linachelewa alifanya maamuzi ya haraka ya kukubali ofa ya kwenda katika klabu ya KMC inayoshiriki ligi Daraja la Kwanza kwaajili ya msimu ujao unaotarajiwa kuanza karibuni.
Alikuwa ni kati ya mawinga bora katika kikosi cha Lyon lakini kuchelewa kwa ofa kulimsukuma kutua katika klabu hiyo ya ligi daraja la kwanza, kwa kuhofia kukosa usajili baada ya dirisha kukaribia kufungwa

0 comments:

Post a Comment