Rais wa La Liga
Javier Tebas amedai klabu za Paris St-Germain na Manchester City
zilifanya udanganyifu wa kifedha wakati wa kipindi cha kuhama wachezaji.
Akiongea
katika kongamano la Soccerex mjini Manchester, Tebas amesema klabu hizo
zilitumia pesa ambazo hazikuwa zimetokana na shughuli za soka na kwamba
hatua zinafaa kuchukuliwa kuzuia hilo.Tebas amesema PSG "wanaucheka mfumo" uliopo kuhusu uhamisho wa wachezaji baada ya klabu hiyo kuvunja rekodi ya dunia na kulipa £200m kumchukua Neymar kutoka Barcelona.
Alisema: "Tumewafumania wakienda haja ndogo kwenye kidimbwi cha kuogelea. Neymar alienda haja kutoka kwenye ubao wa kurukia. Hatuwezi kukubali hili."
Mkuu huyo wa ligi kuu ya Uhispania aliongeza: "Na si PSG pekee mbali pia Manchester City. Ninahitaji pesa zaidi kutoka kwenye Runinga, la sivyo Manchester City na pesa zao za mafuta watawachukua wachezaji wote."
Shirikisho linalosimamia soka Ulaya Uefa linachunguza PSG kubaini iwapo walivunja sheria za uchezaji haki kifedha.
Hata hivyo hawajaanzisha uchunguzi dhidi ya man City licha ya wito wa La Liga kwamba wafanye hivyo.
City wanamilikiwa na Abu Dhabi United Group tangu 2008 nao PSG wamemilikiwa na serikali ya Qatar, kupitia mfuko wake wa uwezekezaji katika soka tangu 2011.
Tebas amepinga wazo la kutetea klabu hizo kwa kudai kwamba Real Madrid na Barcelona wamewahi kuadhibiwa awali.
"Hilo ni wazo ambalo watoto wadogo wanaweza kutumia," amesema. "Mbona unawapa biskuti na hunipi mimi?"
City ndio waliotumia pesa nyingi zaidi sokoni, £215m ambapo walinunua Kyle Walker (£45m), Bernardo Silva (£43m), Ederson Moraes (£35m) na Benjamin Mendy (£52m).
PSG walinunua Neymar na pia wakamchukua Kylian Mbappe kwa mkopo kutoka Monaco, ambapo wanatarajiwa kumchukua kwa mkataba wa kudumu kwa £165.7m mwaka 2018.
Tebas amesema hawezi kusema kwa uhakika kwamba Cristiano Ronaldo na Lionel Messi hawatawindwa na PSG karibuni.
0 comments:
Post a Comment