Na.Samuel Samuel
Mwezi juni mwakani kwa mara
nyingine tena dunia itashuhudia michuano mikubwa zaidi kisoka iliyoanza
zaidi ya miaka 80 iliyopita . Hii ni michuano ya kombe la dunia ambayo
hufanyika kila baada ya miaka minne . Mwakani itafanyikia nchini Urusi .
Barani Ulaya, Latin America na
Asia tayari wameanza kupata baadhi ya wawakilishi wao baada ya baadhi ya
nchi kufuzu katika makundi yao tayari kwa michuano hiyo mwakani. Latin
ni Brazil na Mexico tayari wamekata tiketi huku barani Ulaya ni Ubelgiji
na wenyeji Urusi . Asia ni Iran .
Barani Afrika bado ni vita kali
kuelekea michuano hiyo . Mwisho wa juma zimepigwa mechi mbalimbali
katika harakati za kutafuta nafasi za kwenda Urusi.
Kundi A; Libya walifanikiwa kupata
ushindi wao wa kwanza dhidi ya Guinea katika uwanja wao wa nyumbani wa
Stade Mustapha Ben Jannet. Waliwatandika Guinea 1-0 na kufanikiwa kupata
alama tatu ingawa bado wanaburuza mkia kundi A wakiwa na alama hizo
tatu huku Tunisia wakiwa kileleni na alama 9, DRC wanashika nafasi ya
pili wakiwa na alama 6 lakini wakicheza mechi mbili tofauti na Tunisia
waliocheza mechi tatu. Guinea nafasi ya tatu wakiwa na alama 3 sawa na
Libya mkiani.
Mabingwa wa Afrika Cameroon baada
yakula kichapo cha 4-0 jijini Lagos dhidi ya Nigeria ‘ super Eagles ‘ ,
jumatatu walijitutumua na kutoka sare ya 1-1 jijini Younde katika
harakati hizo za kwenda Urusi. Cameroon wanashika nafasi ya tatu kundi B
wakiwa na alama 3 huku Nigeria wakiwa kileleni na alama 10 wakiwa na
mechi mbili tu kukata tiketi ya Urusi. Wamebakiza mechi dhidi ya Zambia
walio nafasi ya pili na alama 4 pia dhidi ya Algeria wanaoburuza mkia
kundi lao wakiwa na alama 1. Kundi hili njia nyeupe kwa Nigeria kwenda
Urusi.
Kundi C kuna Ivory coast waliopo
kileleni na alama 7 huku Morocco wakishika nafasi ya pili kwa alama 5.
Gabon wapo nafasi ya tatu wakiwa na alama 2 huku Mali wakiburuza mkia
kwa alama 1. Timu zote zimecheza mechi tatu . Mchuano mkali hapa ni
Ivory coast dhidi ya Morocco.
Kundi D linaongozwa na Burkinafaso
wenye alama 5 kileleni , Senegal wanashika nafasi ya pili kwa alama 4,
Afrika ya kusini nafasi ya tatu kwa alama 3 na Cape Verde wakiwa mkiani
pia kwa alama 3. Hili kundi bado ni ngumu kwa timu zote kutokana kuwa na
tofauti ya alama 1 mpaka 2 kwa aliyeko juu na mkiani sawa na mechi moja
tu na timu zote zimecheza mechi tatu kila mmoja.
Kundi la mwisho ni kundi E ambalo
linaongozwa na Uganda toka Afrika mashariki wakiwa na alama 7 . Misri
wanashika nafasi ya pili kwa alama 6 na Ghana wakiwa nafasi ya tatu kwa
alama 2. Congo-Brazaville wapo mkiani wakiwa na alama 1. Mtihani mkubwa
kwa vinara wa kundi hili Uganda ni Misri ambao wanatofautiana nao kwa
alama moja ingawa mafarao hao hawana rekodi nzuri ya kufuzu michuano ya
kombe la dunia licha ya ubora wa soka lao Afrika nakuwa na rekodi nzuri
ya kubeba kombe la AFCON . Misri wamewahi kufuzu mara mbili tu katika
michuano ya kombe la dunia . Mwaka 1934 na mwaka 1990. Huu unaweza kuwa
mtaji mzuri kisaikolojia kwa Uganda kupambana vyema na kuweka rekodi
yakuwa taifa la kwanza kutoka Afrika mashariki kufuzu kwa michuano hiyo
mikubwa zaidi duniani. Tayari Uganda walitoa onyo kwa Misri katika mechi
yao ya kundi hili baada ya kuwapiga 1-0 Nambole stadium Uganda kwa goli
la Emanuel Okwi.
Bara la Afrika linatoa timu tano
tu katika makundi hayo matano hivyo kila atakayemaliza wakwanza kwenye
kundi ndio mwakilishi wa Afrika mwakani huko nchini Urusi.
0 comments:
Post a Comment