Wednesday, November 29, 2017

BARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limetaua marefa wawili tu wa Tanzania kwa ajili ya michuano ya Kombe la Challenge inayotarajiwa kuanza Desemba 3 hadi 16, mwaka huu nchini Kenya. 
Hao ni mpuliza kipyenga Heri Sasii na mshika kibendera Soud Lila, wote wa Dar es Salaam ambao wanatarajiwa kuondoka nchini kesho kwenda Kenya kwa ajili ya kazi hiyo.
CECAFA pia imemteua kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania na Bara, Sunday Kayuni aliyewahi pia kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF kuwa Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi pamoja na Mtanzania mwingine, Ahmed Iddi Mgoyi.
Heri Sasii (kulia) kwa pamoja na mshika kibendera Soud Lila wameteuliwa kuchezesha CECAFA Challenge 2017 nchini Kenya

Mgoyi, Mjumbe Mteule wa Kamati ya Utendaji ya TFF kwa pamoja na Kayuni aliyewahi kufundisha klabu maarufu Tanzania, Yanga wanatarajiwa pia kuondoka kesho kwenda Kenya.  
CECAFA Challenge ndiyo michuano mikongwe zaidi ya soka barani Afrika ambayo ilianza mwaka 1926 ikijulikana kama Kombe la Gossage hadi mwaka 1966, ilipobadilishwa na kuwa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati hadi mwaka 1971 ilipobadilishwa tena na kuwa CECAFA Challenge.
Wadhamini tofauti wamekuwa wakiingia na kutoka kwa kipindi chote hicho, lakini taarifa zinasema kuanzia mwaka huu Televisheni namba moja Afrika Mashariki na Kati, Azam TV ndiyo wanakuwa wadhamini wapya ambao pia watakuwa wanarusha moja kwa moja michuano hiyo. 
Uganda ndiyo mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo tangu mwaka 1971, wakiwa wamelitwaa mara 14, wakifuatiwa na Kenya mara sita, Ethiopia mara nne na Tanzania mara tatu.
Uganda, The Cranes pia ndiyo mabingwa watetezi wa michuano hiyo baada ya kutwaa taji la michuano hiyo mwaka 2015 nchini Ethiopia wakiwafunga Rwanda 1-0 kwenye fainali mjini Addis Ababa, wakati mwaka jana michuano hiyo haikufanyika kwa sababu ya kukosa nchi mwenyeji. 

0 comments:

Post a Comment