Ni ile ya Ajib, Okwi, Asante Kwassi, Kiduku ipi ‘free kick’ bora zaidi VPL hadi sasa?
MSHAMBULIZI Mganda, Emmanuel Okwi anaongoza chati ya ufungaji bora katika ligi kuu Tanzania Bara. Kufikia raundi ya 11 kwa kila timu Okwi amefanikiwa kufunga magoli nane, huku kwa karibu akifuatiwa na Mzambia, Obrey Chirwa anayechezea Yanga SC na mshambulizi kijana Mohamed Rashid anayekipiga Tanzania Prisons-wawili hao wawefunga magoli sita kila mmoja.
Katika michezo saba ya mzunguko wa 11 ni klabu tatu tu ambazo zilifanikiwa kupata matokeo ya ushindi. Hakuna timu iliyokuwa ugenini ambayo ilifanikiwa kupata ushindi huku vigogo wote wane katika ligi vinara Simba SC, Yanga, Azam FC na Mtibwa Sugar FC zikishindwa kupata matokeo.
Kikubwa ambacho nimetokea kuvutiwa nacho katika michezo ya Ijumaa, Jumamosi, Jumapili na ule uliokamilisha mzunguko wa 11 jana Jumatatu-nimevutiwa na magoli mawili ya mikwaju ya faulo ambayo yalizizuia Simba na Azam FC kupata ushindi katika viwanja vya vyumbani.
Magoli hayo yaliyofungwa na mlinzi wa kati wa Lipuli FC, Asante Kwassi vs na Kelvin Sabato ‘Kiduku’ vs Azam FC yamenifanya nijiulize ipi ni ‘free kick’ bora zaidi hadi sasa katika VPL. Je, ni ile ya Ibrahim Ajib vs Njombe Mji FC ama Okwi vs Mtibwa Sugar FC?
Njombe Mji 0-1 Ibrahim Ajib
Si tu Ibrahim Ajib alikuwa akiifungia Yanga goli lake la kwanza tangu alipojiunga nayo Agosti mwaka huu, bali kijana huyu anayevaa jezi namba kumi alifunga goli pekee ambalo liliwapa mabingwa hao mara tatu mfululizp na watetezi wa taji ushindi wa kwanza msimu huu katika wiki ya pili tu.
Yanga ilikuwa imetoka kuvutwa shati na Lipuli FC katika uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na safari yao ya kwanza mkoani walikwenda kucheza katika uwanda wa baridi kali. Walikuja kushinda kwa mpira ambao haukutegemewa na yeyote yule labda Ajib mwenyewe ambaye akiwa mbali kabisa yapata mita zaidi ya 25 katika wing ya kushoto alipisha mpira juu ya ukuta na kiki yake kali ilijaa nyavuni moja kwa moja.
Mechi ilionekana kuwa ngumu huku kikosi cha Lwandamina kikicheza bila maelewano mazuri kati ya washambuliaji Donald Ngoma na Ajib wakapata mkwaju wa faulo dakika ya 16’ na hapo ndipo ‘Pele wa Jangwani’ alipofunga goli la kwanza kwa klabu yake mpya huku pia likiwa ni goli la kwanza kufungwa kwa mpira wa faulo msimu huu.
Emmanuel Okwi 1-1 Mtibwa Sugar
Mganda, Okwi alifunga goli lake la saba katika ligi na kuinusuru timu yake ya Simba kuchapwa kwa mara ya kwanza msimu huu, tena wakicheza nyumbani ( Uhuru Stadium) Mtibwa walitangulia kufunga mapema tu mwa mchezo kupitia Stamil Mbonde na stahili yao ya kujilinda ilikuwa bora hadi pale kiki ya mwisho kabisa katika mchezo ilipowanyima ushindi wa kwanza vs Simba katika ardhi ya Dar es Salaam baada ya kusubiri kwa zaidi ya muongo mmoja.
Mashabiki wa Simba baadhi waliamua kuondoka uwanjani wakati mwamuzi wa akiba alipoonyesha dakika tatu za nyongeza. Waliamini safu ya ulinzi wa golikipa Benedict Tuinocco, Salum Kanoni, Issa Rashid, Dixon Daud na Kassian Ponela iliweza kuwazua washambuliaji wao hatari lakini kwa wachezaji ilikuwa ni tofauti-waliendelea kupeleka mpira katika lango la Mtibwa kadri ilivyowezekana na presha yao ikasababisha mlinzi Erasto Nyoni kufanyiwa madhambi karibu na eneo la mita 18.
Okwi akauchukua mpira ule, akajenga utulivu mkubwa na naamini alijenga mawazo kuwa baada ya kiki yake mwamuzi atamaliza pambano kwani hata zile dakika tatu za nyongeza zilionekana kumalizika. Nini kilitokea? Kiki moja maridadi sana ikaenda moja kwa moja nyavuni na Simba wakakomboka katika ‘muda maalum’
Simba 1-1 Asante Kwassi
Wakati nilipompanga mlinzi huyu wa kati katika kikosi change bora cha msimu uliopita kuna watu walihoji, na nilipopendekeza kusajiliwa Yanga kwa mlinzi huyo mara baada ya kumalizika kwa mkataba wake na Mbao FC pia kuna watu walikebehi, lakini siku zote nimeona kitu kikubwa kutoka kwa raia huyu wa Ghana.
Kwanza ni kiongozi, anatumia akili nyingi sana wakati anapozuia, ana uwezo wa juu wa kuanzisha pasi za mashambulizi zaidi ana ufahamu mkubwa sana kuhusu usomaji wa mchezo na mchezo wenyewe wa soka. Ni rah asana kutazama safu ya walinzi watatu wa Lipuli FC pale kati, Mganda, George Owino, Kwasi na Novaty Lufunga. Yanga, Azam FC wote waliangaika sana walipokutana na Lipuli na yote sababu ya Mghana huyu.
Kabla ya mchezo wao wa Jumapili iliyopita vs Simba, Kwassi alikuwa ameshafunga magoli manne lakini goli lake la tano lilikuwa ‘bab-kubwa’ na lilionyesha funzo linguine kwa wapigaji wa mipira iliyokufa. Licha ya Simba kutangulia kufunga utulivu na hamasa ambayo Kwassi alikuwa nayo ilinifanya niendelee kumfutilia mchezaji huyo.
Alipoenda kupiga mkwaju wa faulo nilimwambia jirani yangu tuliyekuwa tukitazama pamoja mechi ile “ kama ni mpigaji mzuri hii ni nafasi ya goli, na mahala pekee ambako mpira unapaswa kupita ni katika upenyo ambayo utatengenezwa na mchezaji wa Lipuli ama kuupitisha mpira juu ya ukuta”
Kikawaida golikipa utegemea ukuta kuzuia mpira wa faulo hivyo yeye ukaa upande wa pili hivyo ikitokea mpigaji mzuri akapiga kama alivyofanya Kwassi hata kipa anayetajwa bora kama Aishi Manula hawezi kuufikia mpira huo ikiwa utavuka ukuta au kupenyezwa katika upenyo. Kwassi alifunga goli lake la tano lakini likiwa ni la kusawazisha kwa timu yake katika mchezo uliomalizika kwa sare ya kufungana 1-1.
Azam 1-1 Kelvin Sabato
Si tu alikuwa akiisawazishia timu yake ya Mtibwa Sugar goli bali ilikuwa ni sawa na kusawazisha katika ‘vita ya faulo’ kati ya wachezaji wazawa na wale wa kimataifa. Baada ya Okwi na Kwassi kufunga magoli muhimu ya kusawazisha kwa timu zao, Kiduku naye aliungana na Ajib kuwa mchezaji wa pili mzawa kufunga kwa mpira wa faulo.
Azam FC ilipata goli la kuongoza mara baada ya kuanza kwa kipindi cha pili lakini dakika ya 72’ Kiduku ambaye alitokea benchi alifunga goli moja kali sana la mkwaju wa faulo akiwa nje kidogo ya eneo la mita 18. Alijenga utulivu mkubwa na kupiga kiufundi mpira uliopita juu ya ukuta wa wachezaji wa Azam FC na ilikuwa ngumu sana kwa golikipa wao Mghana, Razack kufanya chochote zaidi ya kuishia kutazama tu mpira huo ukitikisa nyavu zake.
Kama umefanikiwa kuona michezo hii minne iliyotoa magoli haya ya mikwaju ya ‘freekick’ ipi ilizaa goli la kupendaza zaidi japokuwa yote manne yalikuwa bora. Upande wangu nimevutiwa zaidi ya goli la Kwassi vs Simba, wewe, je?
0 comments:
Post a Comment