Mataifa ambayo
yamefuzu kwa Kombe la Dunia mwaka ujao nchini Urusi mwaka ujao
yatafahamu yatakutana na nani hatua ya makundi droo itakapofanyika leo
Urusi.
Kombe hilo la Dunia litashirikisha timu 32, na michezo itachezwa kati ya 14 Juni na 15 Julai.Afrika inawakilishwa na Misri, Nigeria, Morocco, Tunisia na Senegal.
Mataifa yaliyofuzu
Kuelekea zoezi hilo baadhi ya timu zimepangwa kwenye vyungu, chungu cha kwanza ambacho kina timu mwenyeji Urusi, Ujerumani, Brazil, Ureno, Argentina, Ubelgiji, Poland na Ufaransa.
- Mambo muhimu kuhusu nchi ambazo tayari zimefuzu Kombe la Dunia 2018
- Taifa la watu 335,000 lafuzu Kombe la Dunia
Vyungu vimepangwa vipi?
Vyungu Kombe la Dunia | |||
---|---|---|---|
Chungu 1 | Chungu 2 | Chungu 3 | Chungu 4 |
Urusi (wenyeji) | Uhispania (8) | Denmark (19) | Serbia (38) |
Ujerumani (1) | Peru (10) | Iceland (21) | Nigeria (41) |
Brazil (2) | Uswizi (11) | Costa Rica (22) | Australia (43) |
Ureno (3) | England (12) | Sweden (25) | Japan (44) |
Argentina (4) | Colombia (13) | Tunisia (28) | Morocco (48) |
Ubelgiji (5) | Mexico (16) | Misri (30) | Panama (49) |
Poland (6) | Uruguay (17) | Senegal (32) | Korea Kusini (62) |
Ufaransa (7) | Croatia (18) | Iran (34) | Saudi Arabia (63) |
Droo ya michuano hiyo itafanyika Ijuma, tarehe 1 Desemba katika ukumbi wa State Kremlin Palace jijini Moscow kuanzia saa kumi na mbili jioni Afrika Mashariki.
Msimamizi wa droo hiyo atakuwa mshambuliaji wa zamani wa England Gary Lineker ambaye alicheza Kombe la Dunia 1986 na 1990. Atasaidiana na mwanahabari wa michezo kutoka Urusi Maria Komandnaya.
Timu zimepangwa kwenye vyungu kwa kufuata viwango vya soka vya Fifa mwezi Oktoba 2017.
Kuna vyungu vinne, kila chungu kikiwa na timu nne.
Urusi itakuwa kwenye chungu cha kwanza ikiwa na timu saba zilizoorodheshwa za juu zaidi. Timu nane zinazofuata zitakuwa kwenye chungu vya pili, zinazofuata kwenye chungu nambari tatu na zilizoorodheshwa chini zaidi ziwe chungu cha nne.
Hakuna timu kutoka shirikisho moja, ila Uefa pekee, zinaweza kupangwa kundi moja.
Kunaweza kuwa na timu mbili pekee za kutoka Ulaya katika kundi moja.
Wageni watakaohudhuria droo hiyo watashirikisha mmoja kutoka kila taifa kati ya nchi nane ambazo zimeshinda Kombe la Dunia.
Kutakuwa na Laurent Blanc (Ufaransa), Gordon Banks (England), Cafu (Brazil), Fabio Cannavaro (Italia), Diego Forlan (Uruguay), Diego Maradona (Argentina), Carles Puyol (Uhispania) na Miroslav Klose (Ujerumani)
Nani wanapigiwa upatu kushinda?
Mabingwa watetezu Ujerumani wanapigiwa upatu kushinda, wakifuatwa na Brazil, Uhispania, Argentina, Ufaransa, Ubelgiji na kisha England.Ujerumani chini ya Joachim Low wanatafuta kuwa nchi ya kwanza kushinda Kombe la Dunia mtawalia tangu Brazil wakiwa na Pele 1958 na 1962.
Nani alivutia zaidi mechi za kufuzu?
Ujerumani hawajashindwa mechi hata moja ya fainali za au za kufuzu kwa Kombe la Dunia tangu nusu fainali ya 2010 dhidi ya Uhispania.
Walimaliza michuano ya kufuzu 2018 wakiwa wameshinda mechi 10 kati ya kumi walizocheza, na kufunga mabao 43. Walifungwa mara nne pekee.
Ubelgiji, Uhispania na England wote walimaliza mechi za kufuzu Ulaya bila kushindwa.
Brazil walitamba mechi za kufuzu Kombe la Dunia - lakini baada ya kumuondoa meneja Dunga na kumuingiza Tite.
Barani Asia, Iran walipitia makundi mawili bila kushindwa - mechi 18 bila kushindwa, ambapo mechi 12 kati ya hizo hawakufungwa bao hata moja.
Morocco walifuzu bila kufungwa bao hata moja katika kundi lao la kufuzu Afrika, ambapo walimaliza juu ya Ivory Coast.
Nani wanacheza mara ya kwanza?
Iceland ndiyo nchi ya kwanza pekee yenye raia ambao ni chini ya milioni moja kuwahi kufika Kombe la Dunia.
Hawakuwa wamefuzu kwa michuano mikubwa kabla ya kushiriki Euro 2016 ambapo waliwalaza England katika safari yao ya kufika robo fainali.
Panama, taifa la Amerika ya Kati, nao walifika Kombe la Dunia baada ya bao la ushindi la dakika ya 88 dhidi ya Costa Rica, bao ambalo pia liliwazuia Marekani kufuzu.
Nani miamba ambao wameachwa nje?
Walioshangaza zaidi walitoka Ulaya.
Mabingwa mara nne Italia walishindwa kufuzu kwa mara ya kwanza tangu 1958 baada ya kuondolewa na Sweden.
Uholanzi pia walishindwa kufuzu.
Jamhuri ya Czech, Wales, Scotland, Austria, Bosnia-Herzegovina na Uturuki ni miongoni mwa nchi nyingine za Ulaya zilizoshindwa kufuzu hatua ya makundi.
Jamhuri ya Ireland, Ireland Kaskazini na Ugiriki pia waliondolewa kwenye mechi za muondoano za kufuzu baada ya makundi.
Jimbo la Concacaf, Marekani walishindwa kufuzu kwa mara ya kwanza tangu 1986.
Barani Afrika, Ivory Coast, Cameroon na Ghana - wote ambao walishiriki Kombe la Dunia Brazil 2014 - pia hawakufuzu.
Chile, walioorodheshwa nafasi ya tisa duniani, pia walishindwa kufuzu.
Tiketi zinauzwaje?
Fifa wamepokea maombi 3.5 milioni ya tiketi, 300,000 yakiwa maombi ya tiketi za mechi ya fainali uwanjani Luzhniki.
Asilimia 57 ya maombi yametoka kwa wakazi wa je ya Urusi.
Tiketi ya bei nafuu zaidi ya fainali Kombe la Dunia ambayo raia asiye wa Urusi anaweza kununua ni ya £345.
0 comments:
Post a Comment