Monday, December 4, 2017

Na Halidi Mtumbuka
Michael Jackson ni moja kati ya wanamuziki waliyoifanya dunia ya wapenda muziki kuupenda maradufu muziki wake. Michael Jackson aliifanya dunia kuwa rahisi mno kwa wapenda muziki na hata wale ambao hawakuzaliwa na vinasaba vya kuupenda muziki kwenye miili yao, walipenda vitu vichache kutoka kwake.
Ni yeye aliyependwa kutokana na aina yake ya uchezaji jukwaani na ni yeye aliyeifanya mioyo laini ya wasichana warembo kuongeza mapenzi yao maradufu kwenye tasnia hiyo. Dunia ilishuhudia mtu aliyeufanya muziki kupenya mioyoni mwa wapenda muziki.
Muigizaji Steven Kanumba aliifanya tasnia ya uigizaji Tanzania kupendwa na hata wasiopenda filamu za Kitanzania. Huyu ni mwanaume aliyeaminika kwamba kaburi lake lilifunika vitu viwili. Cha kwanza ni mwili wake na cha pili ni ubunifu mzima wa tasnia hiyo.
Kuna watu wamezaliwa kwa kazi moja tu duniani, kuifanya kazi yao kupendwa na hata wasiopenda kazi zao. Yupo binaadamu mmoja alienifanya niyakumbuke majina hayo mawili niliyoyataja hapo juu baada ya kuishuhudia kazi nzuri aliyokuwa akiifanya uwanjani na thamani yake hivi sasa baada ya kujiunga na Simba, huyu ni Haruna Niyonzima.
Haruna Niyonzima amebarikiwa uwezo wa kuufanya mpira kupendwa na hata wasioupenda mpira. Ni mmoja kati ya binaadamu wachache wanaozifanya ipasavyo kazi zao na kuwavutia wengine wazipende kazi zao. Ni nani asiyetamani kumuona Niyonzima uwanjani? Ni mrembo gani asiyependa kumuona Niyonzima? Hata kama asipoupenda mpira, atampenda tu Haruna Niyonzima.
Awapo kwenye uwezo wake wa kawaida, huyu ni zaidi ya burudani, miguu yake ni zaidi ya ala za muziki masikioni, mwili wake ni zaidi ya viungo laini vya Michael Jackson kwenye shughuli moja tu, kuufanya mpira utembee atakavyo, niamini Niyonzima bado anaishi. Hajapotea kama mnavyodhani.
Niyonzima anaelewa nini alifanyalo, anajua ni kipindi gani yupo hivi sasa, Simba inahitaji nini na kocha wake anahitaji nini, mashabiki, viongozi na wanachama waandamizi wa klabu hiyo wanahitaji nini ndio maana hucheza zaidi kutafuta matokeo. Presha ni kubwa mno, hebu tumuache kwanza ashushe presha.
Sababu hii ya kutimiza majukumu yake ipasavyo uwanjani na kuwa mwenye muendelezo wa kile bora kutoka kwenye miguu yake ndicho kinachowafanya hata makocha na viongozi wa timu nyingine kutamani kufanya nae kazi kipindi alipokua Yanga. Niyonzima bado anaishi.
Ndio, kwani wakati wa ufunguzi wa dirisha dogo la usajili, timu ambayo ni kifurushi cha kushtua msimu uliopita,Ettiene, Mbao FC ilinukuliwa ikisema inahitaji wachezaji wenye ubora kama wa Niyonzima.
Tunatarajia kuimarisha kikosi chetu kwa kupata wachezaji wenye ubora kama Niyonzima na Mavugo kwa ajili ya mzunguko wa pili” hii ni kauli inayotambua thamani, uwezo na mchango wa binaadamu huyu kwenye mpira.
Mkumbuke Niyonzima wa msimu uliopita, majukummu yake Yanga, watu waliomzunguka kisha shughuli yake uwanjani akiwa huru kufanya atakavyo kwa kuwa Yanga haikua na presha kubwa, haikua ni lazima iwe bingwa kama ambavyo Simba ipo misimu hii miwili. Vuta picha ya ule mchezo dhidi ya JKT Ruvu msimu uliopita.
Ulishuhudia alichokifanya alipotolewa Amissi Tambwe kwenye eneo la ushambuliaji? Aliingia Said Juma Makapu ambaye ni kiungo asilia wa ulinzi. Ungeweza kumshangaa George Lwandamina siku ile na usingeweza kumuelewa milele. Lakini alijua ubora wa mchezaji wake hasa kwenye kupiga pasi za mwisho zinazofungua mianya kwa timu kupata ushindi.
Kilichofuata ni Haruna Niyonzima kupanda juu kucheza kama mshambuliaji namba mbili mwenye majukumu ya kumlisha Donald Ngoma, Simon Msuva na Deus Kaseke waliokuwa wakitokea pembeni na kuitanua idara ya ulinzi ya JKT Ruvu.
Bakari Shime kocha wa JKT Ruvu wakati huo aliingia kwa kukaba mno hasa kwenye idara yake ya ulinzi iliyokuwa na nidhamu mno ya ukabaji kwenye kipindi cha kwanza.
Tulishuhudia sana Msuva na Kaseke wakitumika katika kupandisha mashambulizi. Nidhamu kubwa ya Michael Aidan, Edward Charles na wenziwe ilianza kushuka mara tu baada ya Niyonzima kusogea juu na sekunde chache tu Msuva akapata bao.
Niyonzima ndie aliyekuwa ‘Playmaker’ wa Yanga siku ile. Licha ya kutocheza vizuri kipindi cha kwanza, Yanga walistahili ushindi kwenye mchezo huo. Ndiyo maana baada ya mchezo kocha Lwandamina aliandika kwenye akaunti yake juu ya vijana wa Yanga kushinda.
Lwandamina alisema “Vijana walistahili ushindi” ni kweli. JKT Ruvu hawakuonekana kuwa na mipango ya kutafuta ushindi ikiwemo kushindwa kuutumia uwazi katikati ya Vincent Bossou na Kelvin Yondani ambao mara kwa mara walikuwa wakiacha uwazi katikati yao.
Nilijisemea moyoni mwangu, ahsante sana Haruna Niyonzima kwa kukifungua kitabu cha ‘Mchawi Mweusi’ Bakari Shime. Hata kama huupendi mpira na huipendi Yanga, lazima utazipenda tu pasi za Niyonzima, mijongeo yake na namna anavyofungua kurasa ngumu kusomeka na kuzilainisha. Niyonzima utaishi maisha marefu ya mpira, sijawahi kuwa mtabiri ila acha tuamini kwamba ukifuata miiko ya maisha, utaishi maisha marefu.
Thamani yake uwanjani inakwenda sawa na thamani yake sokoni. Huyu ni nyota anayepanda kila kukicha uwanjani na sokoni, anajua jinsi ya kuifanya kazi yake na thamani ya miguu yake.
Tangu alipotua nchini mwaka 2011, Haruna Niyonzima amekuwa na mafanikio yaliyomwezesha kuongeza dau lake kila anapoongeza mkataba. Huu ni mwaka wake wa saba nchini baada ya kuongeza mkataba mara mbili jambo linalomfanya kuwa mchezaji wa kigeni aliyedumu zaidi katika klabu ya Yanga kisha kutimkia Simba.
Mengi yamesemwa kuhusu Niyonzima lakini ukweli unabaki kuwa yeye ni mmoja wa wachezaji wa kigeni waliovuna mamilioni katika soka la Tanzania. Kwa hesabu za haraka haraka tena bila kujumlisha posho na marupurupu mengine, Niyonzima amevuna zaidi ya shilingi milioni 680 katika malipo ya usajili na mishahara yake.
Dau la dola elfu 30 na mshahara wa dola 1500 ulimng’oa APR mwaka 2011 kwa mkataba wa miaka miwili. Mwaka 2013, dau lake lilipanda zaidi baada ya kufanikiwa kuongeza mkataba wa miaka miwili tena kwa kitita cha dola elfu 75 na mshahara wa dola 2500 kwa mwezi.
Mwaka 2015, wakati wengi wakiamini uwezo wake umepungua, Niyonzima alionesha umakini kwenye mazungumzo ya kuongeza mkataba kwa kutamka wazi kuwa yuko tayari kutua Simba au Azam.
Kwa namna fulani, jambo hilo lilimsaidia kupewa mkataba wenye maslahi zaidi. kwa mshahara unaotajwa kuwa dola elfu 3000 na dau la dola 60,000 alianguka saini ya kuendelea kuvaa jezi za rangi ya kijani na njano kwa miaka miwili zaidi.
Licha ya mapungufu yake mengine ndani na nje ya uwanja, Niyonzima amekuwa akipanda dau kwa sababu ya kujiamini na kutambua ‘wakati wa kupambania maslahi yake kwa kuonesha kiwango cha kuwafunga mdomo wakosoaji’.
Mwaka 2013, akijua kabisa mkataba wake unaelekea ukingoni alionesha kiwango cha hali ya juu ikiwemo kufunga bao tamu na la ushindi dhidi ya Azam. Msimu uliopita tena, hasa katika mechi tano za mwisho Niyonzima anaonesha ni jinsi gani alistahili kuendelea kuwepo Tanzania.
Kwa sasa anavuna mkwanja mrefu mno ndani ya klabu ya Simba, hata kama mkimbeza tayari ameshachukua chake na siku yoyote akihitajika kuondoka atafanya hivyo, lakini amini nikwambie, ipo siku tutamshangaa Niynzima maradufu uwanjani.
Nakumbuka kipindi kile alipotaka kuachwa kwa sababu za utovu wa nidhamu. Nimekumbuka tu. Huyu ndie Niyonzima, hakika akiamua kuzilainisha zile kurasa zote zilizongumu kusomeka na kuufanya mchezo wa soka kuwa rahisi mno machoni mwetu, hufanya hivyo bila wasiwasi.

0 comments:

Post a Comment