Monday, December 4, 2017

TANZANIA Bara imeanza kwa sare ya 0-0 na waalikwa kutoka Kaskazini mwa Afrika, Libya katika mchezo wa Kundi A Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge jioni ya leo Uwanja wa Kenyatta, Machakos nchini Kenya. 
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Alex Muhabi aliyesaidiwa na Okelo Dick wote wa Uganda na Kakunze Herve wa Burundi, Libya ndio waliotawala zaidi na kutengeneza nafasi nyingi, lakini bahati mbaya umaliziaji ukawaangusha.
Tanzania Bara, au Kilimanjaro Stars ya kocha Ammy Ninje haikucheza kwa muunganiko wa kitimu zaidi kila mchezaji alicheza kivyake.
Beki wa Tanzania Bara, Gardiel Michael (kulia) akimtoka mchezaji wa Libya, Alharaish Zakaria leo Machakos

Mbaya zaidi sehemu ya kiungo ilizidiwa na haikuwa na ubunifu kabisa, hivyo kuwapa nafasi Libya kutawala.
Angalau baada ya kuingia Jonas Mkude, sehemu ya kiungo ya Kilimanjaro Stars ilianza kucheza vizuri na hapo ndipo walipoanza kufika kwenye eneo la wapinzani na kupeleka mashambulizi kadhaa. 
Katika mchezo wa kwanza wa Kundi A na mashindano kwa ujumla, wenyeji Kenya waliichapa Rwanda 2-0 Uwanja wa Bukhungu, Kakamega, mabao ya Masoud Juma kwa penalti na Otieno Duncan.  Amavubi ilimaliza pungufu mechi hiyo baada ya Kayumba Soter kutolewa kwa kadi nyekundu.
Michuano hiyo itaendelea kesho kwa mechi moja ya Kundi B, Uganda wakimenyana na Burundi Kakamega kuanzia Saa 9:00 Alasiri.
Kikosi cha Tanzania Bara kilikuwa; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gardiel Michael, Kennedy Willson, Kevin Yondan, Hamisi Abdallah/Jonas Mkude dk66, Shiza Kichuya, Ibrahim Ajib, Elias Maguri/Daniel Lyanga dk82, Mbaraka Yussuf/Yahya Zayeddk61 na Muzamil Yassin.
Libya; Abdullah Fathi, Aljamal Tariq, Sabbou Motasem, Ajbarah Saed, Maetoyq Ali, Madeen Muhanad, Albadri Faisal, Taktak Muftah/Almryamu Khaled dk60, Mohamed Amer, Alharaish Zakaria/Aleyat Mohamed dk79 na Saeid Saleh/Tubal Mohamed dk69.

0 comments:

Post a Comment