Monday, December 4, 2017


KOCHA wa Lipuli FC, Suleiman Matola amesema kwamba atasajili wachezaji watano katika dirsha dogo kuimarisha kikosi chake katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. 
Akizungumza na blog hii  leo kwa simu kutoka Iringa, Matola amesema kwamba alichelewa kujiunga na timu mwanzoni mwa msimu, hivyo hakupata muda wa kutosha wa kusajili. 
“Tuliingia kwenye Ligi Kuu baada ya kusajili kwa siku mbili tu, hivyo hatukupata aina ya watu wote tuliowataka, lakini sasa tunataka kutumia kipindi hiki cha dirisha dogo kurekebisha mambo,”amesema Matola.
Suleiman Matola anataka wachezaji watano wapya kuimarisha kikosi chake katika Ligi Kuu 

Matola aliyewahi pia kuchezea SuperSport United ya Afrika Kusini amesema anahitaji mawinga wawili, kiungo mchezeshaji mmoja na washambuliaji wawili, ili Lipuli itishe katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.
Nahodha huyo wa zamani wa Simba SC amesema kwamba amewasilisha majina matano ya wachezaji anaowataka wasajiliwe dirisha dogo wakiwemo winga Jamal Mnyate na mshambuliaji Juma Luizio anaowataka kwa mkopo kutoka Simba SC.
Matola pia anamtaka mshambuliaji wa zamani wa Simba, Muivory Coast, Frederick Blagnon ambaye amerejea kwao bada ya kuondoka Msimbazi kufuatia kufanya kazi kwa msimu mmoja. 
Kwa sasa Lipuli FC inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa pointi zake 14 baada ya kucheza mechi 11, ikizidiwa pointi tisa na vinara Simba SC. 

0 comments:

Post a Comment