Saturday, December 2, 2017

KLABU ya Yanga imetetea hatua yake ya kusajili wachezaji vijana wadogo ikisema kwamba inataka wakulie ndani ya utamaduni wa klabu hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika amesema leo mjini Dar es Salaam kwamba klabu inahitaji vijana ambao watakulia ndani ya klabu na kujua misingi na utamaduni wa klabu kabla ya kuwa wachezaji wakubwa baadae.
Na Mwenyekiti huyo wa Usajili amesema hayo kufuatia klabu kumsajili mshambuliaji chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Yohanna Oscar Nkomola.
"Tunahitaji kuwa na vijana ambao watakuwa wakiwa ndani ya klabu, hii itawafanya kujua misingi na utamaduni wetu kabla kuwa wachezaji wakubwa baadae. (Nkomola) ana kipaji kikubwa, ni jukumu la benchi la ufundi kukiendeleza kwa manufaa ya klabu siku za usoni,” amesema Nyika..
Yohanna Nkomola (kulia) akipeana mikono na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika baada ya kukamilisha usajili wake wiki hii

Nkomola anayesimamiwa na akademi ya Cambianso ya Dar es Salaam amesaini mkataba wa miaka miwili huo mapema wiki hii kabla ya kwenda Kenya na kikosi cha Tanzania Bara kwenye michuano ya Kombe la CECAFA Challenge. 
Kwa kusaini Yanga, Nkomola anakuwa mchezaji wa tatu kutoka kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys kilichoshiriki Fainali za Vijana za U-17 Afrika nchini Gabon mwezi Mei mwaka huu. 
Wengine ni kipa Ramadhani Kabwili na kiungo Mussa Said ambao wote wanasajiliwa kama wachezaji wa kikosi cha pili kinachoundwa na vijana chini ya umri wa miaka 20, watakaokuwa wanakomazwa pia kikosi cha kwanza.
Septemba mwaka huu Nkomola alisema amefaulu majaribio katika klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia na atatakiwa kuanzia timu ya vijana hadi atakapofikisha umri wa miaka 18 Aprili mwakani ndipo atasaini mkataba rasmi na kuanza kuchezea timu ya wakubwa.
Hata hivyo, wamiliki wa mchezaji huyo, Cambianso wameona bora ajiunge na Yanga kuliko kurejea  Etoile du Sahel.
Tayari Nkomola ameanza kukomazwa kwenye timu ya wakubwa ya Tanzania na alikuwemo kwenye kikosi cha Taifa Stars ikitoa sare za 1-1 katika mechi zake mbili zilizopita dhidi ya Malawi Dar es Salaam na Benin mjini Coutonou.
Na wakiwa kambini kwa maandalizi ya mchezo dhidi ya Malawi, Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta alimsifu kijana huyo na akamtabiria atafika mbali akiongeza juhudi.

0 comments:

Post a Comment