Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amepokea kwa masikitiko
taarifa ya kifo cha Mwanamichezo nguli Ndg. Athuman Juma Chama
kilichotokea jumapili usiku tarehe 07 Januari, 2018 katika Hospitali ya
Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Akielezea kifo cha marehemu Chama,
Dkt. Mwakyembe amesema kifo chake ni pigo kubwa kwa sekta ya michezo
hususani mchezo wa mpira wa miguu nchini ambayo marehemu alihudumu kwa
umahiri wa hali ya juu na kujijengea jina na heshima miongoni mwa vijana
wapenda soka na Watanzania kwa ujumla.
Dkt. Mwakyembe ametoa pole kwa
familia, Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Baraza la Michezo
Tanzania (BMT), ndugu, jamaa, marafiki na wanamichezo wote nchini na
kuwaombea Mungu awape faraja katika kipindi hiki kigumu cha msiba.
Kipindi cha uhai wake marehemu
Ndg. Chuma (Maarufu kama Jogoo) alichezea vilabu vya Nyamaume Football
Club, Pamba ya Mwanza, Copu United, Mzizima United, Yanga na Timu ya
Taifa (Taifa Stars) aliyoitumikia kwa juhudi kubwa kabla ya kustaafu
kucheza soka mwaka 1988. Hadi anafikwa na umauti marehemu Chama alikuwa
mweka hazina wa Chama cha Wanasoka Tanzania mkoa wa Temeke (SPUTANZA)
Imetolewa na:
Octavian F. Kimario
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo.
09/01/2018.
0 comments:
Post a Comment