Monday, January 8, 2018


SAFARI ya Simba SC katika michuano ya Kombe la Mapinduzi imeishia kwenye hatua ya makundi baada ya kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa URA ya Uganda jioni ya leo Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Kwa matokeo hayo, Simba inamaliza nafasi ya tatu kwenye Kundi A, ikijikusanyia pointi nne katika mechi nne, baada ya kushinda mechi moja dhidi ya Jamhuri 3-1, sare moja na Mwenge 1-1 na kufungwa 1-0 mara mbili na Azam FC na URA.
URA inapanda kileleni mwa Kundi A ikifikisha pointi 10 baada ya kushinda mechi tatu na sare moja, wakati Azam FC iliyoshinda mechi tatu na kufungwa moja inamaliza nafasi ya pili. 
Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Mrundi Masudi Juma (kushoto) akiwa na Kocha wa makipa, ambaye ndiye Msaidizi wake kwa sasa, Muharami Mohammed 'Shilton' 
Bao la URA limefungwa na Deboss Kalama dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya kutimia dakika 45 za kipindi cha kwanza akiingia na mpira kwa kasi kutokea nyuma na kumlamba chenga beki Erasto Nyoni mwanzoni mwa boksi hadi akakaa chini kabla ya kujivuta mbele na kupita shuti la chinichini lililompita kipa Emmanuel Mseja upande wake wa kulia. 
Na bao hilo lilikuja baada ya mabadiliko yaliyofanywa kipindi cha kwanza na kocha Paul Nkata akimpumzisha mshambuliaji Moses Sseruyide na kumuingiza kiungo Hudu Mbulikyi dakika ya 36.
Na hiyo ilitokana na Simba SC kuonekana kutawala zaidi sehemu ya kiungo, hivyo mwalimu wa timu ya Mamlaka ya Mapato Uganda akaamua kupunguza mshambuliaji na kuweka kiungo ili wapunguze utawala wa wapinzani wao uwanjani.  
Simba walicheza vizuri kipindi cha kwanza wakitawala sehemu ya kiungo na kutengeneza nafasi nyingi, lakini wakakosa maarifa ya kufunga tu.
Kipindi cha pili, kaimu Kocha Mkuu, Mrundi Masudi Juma alifanya mabadiliko akiwatoka Nicholas Gyan, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Muzamil Yassin na Shiza Kichuya na kuwaingiza Yussuf Mlipili, James Kotei, Said Ndemla, Laudit Mavugo na Mohammed ‘Mo’ Ibrahim.
Lakini mabadiliko hayo hayakuweza kupindua matokeo kipindi hicho na URA wakafanikiwa kuwatupa nje Simba SC, ambao kesho sasa watapanda boti kurejea mjini Dar es Salaam kujiandaa na mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Mchezo wa mwisho wa Kundi B unafuatia Saa 2:15 usiku, Yanga SC wakimenyana na Singida United hapa hapa Uwanja wa Amaan.
Yanga na Singida zimekwishafuzu Nusu Fainali na leo zitakuwa zinapambana kuwania uongozi wa Kundi B baada ya wote kushinda mechi zao zote nne za awali.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Emmanuel Mseja, Nicholas Gyan/Yussuf Mlipili dk46, Asante Kwasi, Juuko Murshid, Erasto Nyoni, Jonas Mkude/James Kotei dk46, Mwinyi Kazimoto/Said Ndemla dk46, Muzamil Yassin/Laudit Mavugo dk56, Moses Kitandu, John Bocco na Shiza Kichuya/Mohammed ‘Mo’ Ibrahim dk46.
URA; Alionzi Nafian, Enock Kibumba, Brian Majwega, Allan Munaaba, Patrick Mbowa, Julius Mutyaba, Nicholas Kagaba/Steven Mpoza dk90+2, Deboss Kalama/Jimmy Kulaba dk62, Peter Lwasa/Dennis Kamanzi dk72, Moses Sseruyide/Hudu Mbulikyi dk36 na Shafiq Kagimu.

0 comments:

Post a Comment