KIKOSI cha Simba SC kimerejea mjini leo Dar es Salaam baada ya kutolewa katika michuano ya Kombe la Mapinduzi jana kufuatia kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa URA ya Uganda Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Simba SC sasa inaelekeza nguvu zake katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Simba SC itaanza na Gendarmerie Tnale ya Djibouti katika Raundi ya Awali ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu, mechi ya kwanza ikichezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na marudiano ugenini.
Mashirikisho ya nchi nane tu hayajawasilisha wawakilishi ambayo ni ya Cape Verde, Chad, Eritrea, Namibia, Reunion, Sao Tome and Principe, Sierra Leone na Somalia.
Ikivuka hatua hiyo, Ikivuka hapo, Simba itakutana na mshindi kati ya El Masry ya Misri na Green Bufaloes ya Zambia.
Katika michuano hiyo pia kuna timu za USM Alger ya Algeria, Zamalek ya Misri, Raja Casablanca ya Morocco, Enyimba ya Nigeria, DC Motema Pembe ya DRC, SuperSport United ya Afrika Kusini, Al Ahly Shandy na Al Hilal Obied za Sudan, Club Africain ya Tunisia na Nkana FC ya Zambia.
Simba SC inarejea kwenye michuano ya Afrika mwaka huu tangu iliposhiriki mara ya mwisho mwaka 2013 na kutolewa na Recreativo do Libolo ya Angola katika Raundi ya Kwanza.
Simba jana ilimaliza nafasi ya tatu kwenye Kundi A Kombe la Mapinduzi kwa pointi zake nne ilizovuna katika mechi nne, baada ya kushinda mechi moja dhidi ya Jamhuri 3-0, sare moja na Mwenge 1-1 na kufungwa 1-0 mara mbili na Azam FC na URA.
URA imemaliza kileleni mwa Kundi A kwa pointi zake 10 baada ya kushinda mechi tatu na sare moja, wakati Azam FC iliyoshinda mechi tatu na kufungwa moja inamaliza nafasi ya pili.
Bao la lililoizamisha Simba jana lilifungwa na Deboss Kalama dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya kutimia dakika 45 za kipindi cha kwanza akiingia na mpira kwa kasi kutokea nyuma na kumlamba chenga beki Erasto Nyoni mwanzoni mwa boksi hadi akakaa chini kabla ya kujivuta mbele na kupita shuti la chinichini lililompita kipa Emmanuel Mseja upande wake wa kulia.
URA sasa itakuwa na washindi wa pili wa Kundi B Yanga katika Nusu Fainali, wakati Azam FC itamenyana na vinara wa Kundi B, Singida United.
0 comments:
Post a Comment