Thursday, January 11, 2018


SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) na kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL)  leo wamesaini mkataba wa miaka mitatu wa kuidhamini Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) kupitia Bia ya Serengeti Lite.
Mkataba huo wa wenye thamani ya Shilingi Milioni 450 unaifanya Serengeti Lite kuwa bia ya kwanza kuidhamini Ligi ya Wanawake.
Serengeti Breweries ambao pia wanaidhamini timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars kupitia Bia yao ya Serengeti Premium Lager kupitia Mkurugenzi Mtendaji Hellen Weesie wanaamini udhamini huo utatoa msukumo kwa timu zote nane zilizofanikiwa kuingia hatua ya nane bora katika msimu huu wa pili wa ligi hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji Hellen Weesie (kulia) akisaini mkataba na Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura leo

Weesie amesema siku zote Serengeti wanaamini katika kuendeleza vipaji hasa inapokuja katika michezo ambayo inawaleta pamoja wadau mbalimbali na wanaamini udhamini huo utawavutia mashabiki wa rika mbalimbali.
Makamu wa Rais wa TFF Michael Wambura akizungumzia udhamini huo amesema Serengeti Breweries wanafungua milango kwa wadhamini wengine kupitia udhamini huo wa Bia yao ya Serengeti Lite.
Amesema SBL wameangalia mbali zaidi kuingia kwenye soka la Wanawake kwakuwa hata mkutano mkubwa wa FIFA wa maendeleo ya mpira(FIFA Football Executive Summit) utakaofanyika Tanzania February 22 moja ya ajenda zake ni soka la Wanawake .
“Udhamini huu utakuwa kichocheo kwa soka la Wanawake kukua na tunaamini soka la kina mama litajulikana kama inavyojulikana bia yao na udhamini huu fedha tunayoipata tutaitumia vizuri ” Alisema Wambura.
Kwa upande wa Serikali kupitia Afisa Mkuu wa Michezo Henry Lihaya wamesema Makampuni mengine yaige mfano wa SBL kuingia kwenye michezo ambako ni chanzo cha ajira.
Naye mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Wanawake Tanzania(TWFA) Amina Karuma amesema udhamini huo wanaupokea kwa furaha kubwa kwakuwa utasaidia kutimiza lengo kwa mpira wa Wanawake kuchezwa kwa ufanisi.

0 comments:

Post a Comment