Wednesday, January 3, 2018


Mara tu baada ya Rais wa TFF Rais Wallace Karia kutangaza ujio wa ugeni wa FIFA nchini kwa ajili ya kufanya mkutano mkubwa, tayari Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamisi Kigwangala amechungulia fursa.
February 22, 2018 Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa FIFA ‘FIFA Summit’ kwa mara ya kwanza katika historia Tanzania ikiwa mwenyeji.
Waziri Kigwangala amesema, hiyo ni fursa kubwa kwa upande wa Wizara yake kutangaza utalii na vivutio mbalimbali vilivyopo nchini na ataandaa ‘package’ maalum kwa ajili ya wageni hao endapo watapenda kutembelea mbuga za wanyama na vivutio vingine.
“Tumefarijika sana sisi wadau wa utalii kwa sababu wizara yetu inasimamia mambo mbalimbali ikiemo kuvutia watalii kuja nchini kuitangaza nchi yetu kama kivutio cha kipekee cha utalii. Ndani ya utalii kuna Nyanja mbalimbali ambazo zinahusika kuna utalii ambao tumeuzoea wa safari kwa maana ya kwenda kwenye mbuga za wanyama lakini pia tunautalii wa utamaduni, utalii wa ndani na utalii wa mikutano ‘conference tourism’.”
“Ujio wa ndugu zetu wa FIFA kuja kufanya mkutano mkuu wa kimataifa nchini maana yake tunafaidika kwa kiasi kikubwa sana kwenye sekta hii ya utalii. Faida kubwa ya kwanza ambayo tunaipata ni kwamba, ujio wa FIFA unaitangaza nchi yetu kwa hiyo watu wote ambao ni wapenzi, washabiki na wafuatiliaji wa mambo ya soka wakijua kwamba mkutano mkubwa wa FIFA unafanyikia Tanzania wataanza kujiuliza kuna nini Tanzania hadi FIFA imeamua kwenda kufanya mkutano wake mkuu. Kwetu ni tangazo la bure ‘free PR’.”
“Mkutano huu wa FIFA utaongeza imani ya watu juu ya Tanzania watu wengi wataamini kuna amani, kuna miundo mbinu ya kutosha ya kufanya mikutano lakini pia kufanya mambo mbalimbali kwa hiyo nao watatamani walete mikutano yao hapa nchini kutokana na imani watakayoipata kwa sababu FIFA ni taasisi kubwa duniani na imeleta mkutano hapa Tanzania.”
“Tutafaidika na fedha za kigeni ambazo watazitumia hapa, wakiwa hapa watalala kwenye hoteli, watakula vyakula vya hapa lakini pia wanaweza wakatamani kwenda kwenye mbuga za wanyama wanaweza kutamani kununua bidhaa zinazotengenezwa hapa kwa ajili ya kupelekea ndugu zao.”
“Nimeona niwaalike kutembelea mbuga za wanyama na vivutio mbalimbali vya utalii kama beach na maeneo mbalimbali ya kumbukumbu na historia tuliyonayo hapa nchini maeneo ya utamaduni ili wakienda huko kwao wawe mabalozi kwa wenzao. Nitatengeneza ‘package’ maalum kuwapa kama ofa endapo watapenda kwenda kutembea kwenye maeneo hayo ya utalii.”

0 comments:

Post a Comment