Thursday, March 8, 2018


BAO pekee la winga wa kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva usiku wa jana limeipa Difaa Hassan El Jadida ushindi wa 1-0 dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Ben Ahmed El Abdi mjini El Jadida, Mazghan, Msuva mchezaji wa zamani wa Yanga ya Dar es Salaam alifunga bao hilo dakika ya nane, ambalo linakuwa la nne kwake katika michuano hiyo msimu huu, kufuatia kufunga hat-trick katika mchezo wa kwanza dhidi ya Benfica Bissau ya Guinea Bissau.
Simon Msuva (katikati) mbele kabla ya mchezo wa jana katika kikosi cha Difaa Hassan El Jadida

Baada ya kazi yake nzuri jana, Msuva alipumzishwa dakika ya 77 akimpisha Bilal El Magri.
Sasa Difaa Hassan Jadida watatakiwa kwenda kuulinda ushindi wao huo mwembamba kwenye mchezo wa marudiano mjini Kinshasa siku 10 zijazo.
Mechi nyingine za kwanza za Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika jana; Gor Mahia ya Kenya ililazimishwa sare ya 0-0 na Etoile du Sahel ya Tunisia, Zanaco ya Zambia ilifungwa 2-1 nyumbani na Mbabane Swallows ya Swaziland, ZESCO United ya Zambia ilifungwa 1-0 na ASEC Mimosas ya Ivory Coast, TP Mazembe ya DRC iliitandika 4-0 Songo, Aduana Stars ya Ghana iliilaza 1-0 ES Setif ya Algeria, Togo Port ya Togo ilishinda 2-0 dhidi ya Al Hilal Omdurman ya Sudan, 1st de Agosto ya Angola ilishinda 1-0 dhidi ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini MFM iliilaza 2-1 MC Alger ya Algeria, Rayon Sports ililazimishwa sare ya 0-0 na Mamelodi Sundowns, wakati mchezo kati ya mabingwa wa Afrika, Wydad Casablanca na  WAC haukufanyika jana.

0 comments:

Post a Comment