Friday, March 9, 2018


Na Baraka Mbolembole
TUMEICHAGUA vita, sasa hatuna budi kupambana kwa nguvu na hali zetu zote ili kushinda ‘vita hii ya magoli ya ugenini.’ Tayari mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga SC wamefanya ‘uzembe‘ mkubwa kwa kukubali wabotswana, Township Rollers kufunga magoli mawili katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, lakini bado wana nafasi ya kulazimisha ‘kuurudisha ndani mguu mmoja uliondolewa‘ katika ligi ya mabingwa Afrika.
Kipigo cha 1-2 walichokipata Yanga siku ya Jumanne hii kwa hakika kimewakatisha tamaa mashabiki wengi wa klabu hiyo bingwa mara tatu mfululizo nchini. Kwani hawakupoteza mchezo kwa bahati mbaya bali kutokana na ubora wa hali ya juu ulioonyeshwa na wapinzani wao Rollers. Yanga waliwekewa mpira chini, wakalazimishwa kukimbiza wapinzani wao kwa muda mwingi wa mchezo na baadaye wakati mechi inaelekea mwishoni wakaonyeshwa uwezo wao mdogo kimbinu, kiufundi na kumiliki mpira.
Kabla ya kuruhusu goli la pili, wachezaji wa Yanga walishuhudia Rollers wakipiga pasi zisizopungua 20 bila wao kugusa mpira. Kunyanyaswa huko si tatizo lakini inaumiza kufanyiwa hivyo na timu kutoka Botswana tena katika ardhi ya nyumbani.
Bado wako vitani
Katika ruandi iliyopita Caf Champions League kuna dakika 180 zilizosisimua zaidi wafuatiliaji na watazamaji. Dakika 90‘ za kwanza zilipigwa nchini Lesotho, wenyeji Bantu FC waliwapokea ‘wababe‘ wa Azam FC msimu uliopita CCC, timu ya Mbabane Swallows kutoka Swaziland. Mechi hiyo ya kwanza ilimalizika kwa matokeo ya Bantu FC 2-4 Mbabane Swallows. Ilionekana tayari Mbabane amemaliza kazi, lakini bila jitihada kubwa za uzuiaji walizozifanya katika mchezo wa marejeano nyumbani kwao Swaziland bila shaka wangekuwa nje ya michuano.
Dakika 90 za pili zilisisimua mno kwani mechi ilimalizika kwa Mbabane Swallows 1-3 Bantu FC. Matokeo ya jumla, 5-5 na Waswaziland wakasonga kwa sheria ya goli la ugenini. Ilikuwa vita hasa ya magoli ya ugenini‘ hivyo nawakumbusha Yanga kuwa wanaweza kufuta magoli hayo ya ugenini huko Gaborone kama watapambana huku wakisahihisha makosa katika beki yao iliyocheza bila kujiamini Jumanne iliyopita.
Wanatakiwa kupandisha ubora, hamasa na hali ya kujiamini katika idara ya kiungo ambayo ilipoteza mpira mara nyingi, kushindwa kuumiliki walau kwa dakika moja. Pia Wanatakiwa waelewe bila kufunga walau magoli matatu ugenini watakuwa nje ya michuano.
Kuendelea kumwamini Ramadhani Kabwili
Mara mia moja kuongozwa golini na golikipa ‘anayefungwa‘ magoli, si yule ‘anayefungisha’ magoli ya kizembe. Ramadhani Kabwili kama hatopata majeraha, anastahili kumaliza msimu huu akiwa kipa chaguo la kwanza Yanga SC mbele ya Mcameroon, Youthe Rostand. Youthe si golikipa mbaya, lakini kwa mchezaji wa kigeni aliyepevuka kama yeye ambaye anatarajiwa kuisaidia timu anaporuhusu magoli rahisi kama yale vs Majimaji FC na Ndanda FC inakuwa inashusha morali ya timu.
Katika michezo mitatu aliyoichezea Yanga kijana Ramadhani Kabwili ameonyesha anaweza kuwa suluhisho la muda wakati huu Beno Kakolanya akiwa amegoma kuichezea timu kutokana na kutolipwa stahiki zake. Kabwili ana uwezo wa kupanga ngome, kuusoma mchezo, kucheza mipira ya wazi. Ni mwepesi kuliko Youthe na jitihada zake golini zinaongeza hamasa kwa wachezaji wenzake. Kuendelea kumwamini kijana huyu wakati huu Youthe akifanya makosa ya kujirudia-rudia kutamjenga na anaweza kuwa chaguo bora na la muda mrefu.

0 comments:

Post a Comment