Thursday, May 24, 2018



Na Tido Ngalika

Kundi la Spora kupitia WhatsApp linaloshabikia klabu ya Simba limemkabidhi beki Shomari Kapombe zawadi ya kiasi cha shilingi laki tano (500,000) kama mchezaji bora wa mwezi Aprili 2018.

Kapombe amekabidhiwa kiasi hicho cha fedha na Kiongozi Mkuu wa kundi hilo, Ally Masaninga pamoja na fremu iliyo na picha yake katika Uwanja wa Bocco Vetarani unaotumiwa na wekundu hao wa Msimbazi kujifua kwa ajili ya mechi za ligi.

Spora wametoa zawadi ya fedha hizo kama sehemu ya kutoa motisha na hamasa kwa wachezaji wa Simba kujituma zaidi Uwanjani ili kuipigania timu iweze kupata matokeo.

Tangu msimu wa 2017/18 uanze, imekuwa ni utaratibu wa kawaida kwa kundi hilo kutoa zawadi ya mchezaji bora kwa kila mwezi inayolenga kutia morali kwa wachezaji.

Zawadi hiyo imetolewa ikiwa Simba ambao ni mabingwa wapya wa ligi msimu huu wakijiandaa kuhitimisha ratiba ya mechi za ligi Kuu Bara ambapo watacheza dhidi ya Majimaji FC Jumatatu ya wiki ijayo.

0 comments:

Post a Comment